Waendesha Mashtaka wa Illinois, Chicago nchini Marekani wamemfungulia Mfalme wa R&B mashtaka 10 katika kesi ya unyanyasaji wa kingono.

Mwanasheria wa Serikali, Kim Foxx jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa R Kelly anatuhumiwa kuwanyanyasa kingono wanawake wanne, watatu kati yao wakiwa wasichana wenye umri chini ya miaka 18. Anadaiwa kufanya makosa hayo kati ya mwaka 1998 na 2010.

Mwanasheria wa mshindi huyo wa tuzo za Grammy, Steve Greenberg amesema kuwa mteja wake ameshtushwa na hatua hiyo na kwamba imemvunja moyo na kumpa msongo wa mawazo. Amesema angejisalimisha polisi usiku wa kuamkia leo.

Greenberg amesema kuwa Kelly aliomba kukaa na waendesha mashtaka ili awaeleze kwanini tuhuma dhidi yake hazina mashiko lakini walikataa.

Kesi dhidi yake imepangwa kutajwa kwa mara ya kwanza Mahakamani Machi 8 mwaka huu. Kwa mujibu wa nyaraka za Mahakama na sheria ya Chicago, endapo atakutwa na hatia katika mashtaka yote anaweza kufungwa jela kwa kipindi cha hadi miaka 70.

Kwa miongo kadhaa sasa, R. Kelly amekuwa akikabiliwa na tuhuma za kuwanyanyasa wanawake kingono. Tuhuma hizo zilichochewa na makala iliyopewa jina la ‘Surviving R Kelly’, ambayo ilisababisha wasanii waliofanya naye kazi kuziondoa kazi hizo kwenye mitandao.

Mwanasheria wake ameeleza kuwa hana wasiwasi kwakuwa anaamini mteja wake hana hatia.

“Nina mteja ambaye hajawahi kutenda kosa lolote, kwahiyo sina kazi kubwa ya kufanya kama mwanasheria ninayetetea watuhumiwa wa makosa ya jinai,” Associated Press wanamkariri Greenberg.

Baada ya kuachiwa kwa ‘Surviving R Kelly’, polisi waliwataka wanawake wanaodai kunyanyaswa kingono na mwimbaji huyo kujitokeza na kuwa tayari kushirikiana na vyombo vya dola kutafuta haki yao.

Uchaguzi Mkuu wa Rais nchini Nigeria kufanyika leo
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Februari 23, 2019