Mzimu wa kashfa ya ufisadi wa fedha za akaunti ya Escrow unaendelea kumtafuna mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka ambaye hivi sasa amejitosa kuwania tena ubunge wa jimbo hilo.

Jana, Profesa Tibaijuka alilazimika kushuka jukwaani alipokuwa akiomba kura za wanachama wa CCM katika kata ya Nshamba wilayani Muleba kama sehemu ya mchakato wa kura za maoni utakaowezesha kumpata mgombea wa kiti cha ubunge kwa tiketi ya chama hicho.

Wananchi wa kata hiyo, walianza kuzomea baada ya Profesa Tibaijuka kupanda jukwaani na kuanza kunadi sera zake. Zomeazomea hiyo iliongezeka huku wananchi hao wakimkejeli kwa kudai kuwa wanahitaji awape viroba ndipo wamsikilize.

“Tunataka viroba ndio tukusikilize,” walisikika wananchi hao.

Kejeli hiyo inafuatia kauli ya Profesa Tibaijuka aliyoitoa Juni 8 mwaka huu baada ya kuzomewa katika kata hiyo hiyo, mbele ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahman Kinana. Tibaijuka alisema kuwa waliomzomea ni vijana waliokodiwa na kupewa viroba na mahasimu wake ili wamzomee akiwa jukwaani.

Baada ya zomeazomea ya jana, Profesa Tibaijuka alieleza kuwa mkutano huo uliandaliwa na kupangwa na wagombea wanne kati ya tisa wanaowania nafasi ya kugombea kiti cha ubunge kupitia CCM, na kwamba wagombea hao waliweka vijana wengi kwa lengo la kumhujumu.

“Wagombea ni tisa, kati yao wanane ni vijana na mimi ni mwanamke pekee tena mwenye umri mkubwa. Hivyo, walifanya fujo wakikinzana na wafuasi wangu katika maeneo ninayokubalika.”

Mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete alimuondoa Profesa Tibaijuka katika nafasi ya Uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kufuatia kashfa ya ufisadi wa akaunti ya Tegeta Escrow.

Bayern Munich Wakamilisha Yao Kwa Vidal
Messi Alimtesa ‘Kweli’ Rais Wa Gabon