Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi amesema kuwa kuanzia sasa mawakili walioko kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na wanasheria wote katika Wizara, Mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi za Serikali watakuwa ni Mawakili wa Serikali.

Ameyasema hayo kabla hajamkaribisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ahutubie wageni waliohudhuria uzinduzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.

“Kwa miaka mingi kumekuwa na ombwe la usimamizi wa wanasheria walio kwenye utumishi wa umma. Maamuzi mengi yamekuwa yakifanyika pasipo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuwa na taarifa. Mambo yanapoharibika ndio Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inataarifiwa ili kuokoa jahazi,” amesema Prof. Kabudi

Aidha, Prof. Kabudi amesema kuwa mashirika yote ya kimkakati kama vile Bandari, TANESCO nayo yataletwa chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuepuka kuitia hasara Serikali hasara.

Hata hivyo, kutokana na  marekebisho hayo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaratibu na kusimamia Mawakili wa Serikali walio katika Ofisi hiyo na wanasheria wote katika Wizara, mamlaka za serikali za mitaa na taasisi za Serikali ambao sasa watakuwa ni Mawakili wa Serikali. Mawakili wa Serikali walio katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali watakuwa chini ya uratibu na usimamizi wa Mkurugenzi wa Mashtaka na Wakili Mkuu wa Serikali.

Amesema marekebisho hayo yanatokana na marekebisho ya muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia matangazo ya Serikali Na. 48, 49 na 50 ya tarehe 13 Februari, 2018.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Agosti 16, 2018
Video: RC Mbeya afanya ziara ya kushtukiza shule ya msingi, ambana walimu mkuu