Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa amezitaka halmashauri zote nchini kutowapa miradi wakandarasi wasio na uwezo kwa kuwa ndio chanzo kikubwa cha matatizo ya miradi mingi ya maji.

Ametoa agizo hilo mara baada ya kupewa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji Kirando, wilayani Nkasi katika mkoa wa Rukwa ambao utekelezaji wake umekwama kwa muda mrefu kutokana na uwezo mdogo wa mkandarasi.

Prof. Mbarawa amepiga marufuku mkandarasi ambaye hana rekodi nzuri ya kukamilisha kazi alizopewa kupewa mradi zaidi ya mmoja.

“Tumeanza kujenga miradi yenye thamani halisi ya fedha tunazowekeza kwenye miradi ya maji, hatutakubali tena wakandarasi wasio na uwezo waendelee kula fedha za walipa kodi. Ni lazima kuanzia sasa tujiridhishe na kila mkandarasi kwa lengo la kuokoa fedha za walipa kodi kwa kuwa na miradi bora na endelevu,’’ amesema Prof. Mbarawa.

Aidha, amesema kuwa atatuma timu ya wataalamu kutoka wizarani ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji (SUWASA), Mhandisi Hamisi Makalla kufanya upembuzi yakinifu upya wa mradi wa Kirando kabla ya kumtafuta mkandarasi atakayeanza kazi hiyo kabla ya mwisho wa mwaka huu

Hata hivyo, ameongeza kuwa ni lazima hatma ya mradi huo ipatikane kwa haraka na atatoa fedha kwa ajili ya mchakato wa upembuzi yakinifu na mradi huo utagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 7.7.

 

Breaking News: Waziri Lugola akizungumza eneo la tukio ajali ya MV Nyerere
LIVE: Aliyeokolewa akiwa hai ajali ya MV Nyerere akisimulia ilivyokuwa

Comments

comments