Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) Prof. Ibrahim Lipumba ameahidi kuandika barua kwa Rais dkt. John Magufuli baada ya msafara wake kuzuiwa na jeshi la polisi wilayani Mkinga mkoani Tanga.

Lipumba amewasili mkoani humo leo, Januari 20, 2020 mkoani Tanga kwa ajili ya ziara ya kikazi ya kuzugumza na wanachama na viongozi wa CUF ambapo alikutana na katazo hilo la polisi.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi wameeleza Lipumba na wenzake hawakutoa taarifa juu ya ujio wa msafara wao wilayani humo.

Baada ya kukumbana na zuio hilo alitii amri lakini akatupia lawama jeshi la polisi kwa kusema kuwa ni haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara na mikutano ya ndani.

“OCD wa wilaya hii ya Mkinga aweze kufuata taratibu, asizuie mikutano ya ndani, kwasababu vyama hivi vimesajiliwa na tunafanya kazi kufuatana na taratibu na sheria ya vyama vya siasa” amesema Prof. Lipumba

Na kusisitiza kuwa “naendelea kutoa wito kwa Rais magufuli na nitachukua hatua ya kuweza kumwandikia barua aweze kuhakikisha kwamba taratibu zote za kisheria zinafuatwa, zinaheshimiwa na vyama vya siasa vinafanya shughuli zake za siasa kwa mujibu wa sheria”

Wizara ya Afya yaingilia kati hatari ya upungufu wa nguvu za kiume nchini
ACT kupinga Mahakamani Serikali kufunga laini za simu