Wanasheria wa Serikali wametakiwa kuhakikisha hukumu zinazotolewa na mahakama baada ya kesi kumalizika ili kuepuka malalamiko kwa wananchi na kuwa na utayari na kukubali mabadiliko ya kiutendaji vinginevyo jamii itawabadili.

Mwanasheria mkuu wa Serikali Prof. Adelardus Kilangi ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akihitimisha kikao kazi cha siku mbili baina yake wakurugenzi wa sheria, wizara, mashirika, mamlaka za tawala za mikoa na serikali za mitaa na taasisi mbalimbali za serikali.

Amesema kumekuwa na malalamiko ya kutokamilika kwa hukumu zinazotolewa na mahakama, kitu ambacho huleta mapungufu na kuongeza kuwa mabadiliko hayo hayana budi kukabiliwa ili kuboresha huduma kwa wananchi.

“Wanasheria wa Serikali tuhakikishe hukumu zinakamilika lakini pia tunalazimika kubadilika na kama tusipobadilika basi tutabadilishwa na jamii tutabadilishwa na mazingira na hii ni kwa wanasheria wote hata mawakili wa kujitegemea,” amebainisha Prof. Kilangi.

Amesema mwananchi huwa anaangalia ni namna gani haki inatendeka kutokana na mambo mbalimbali yanayomgusa maishani mwake ili kujiridhisha namna anavyothaminiwa kwa misingi ya haki hivyo wanasheria hao hawana budi kukubali mabadiliko.

Kilangi amebainisha kuwa katika utumishi wa umma serikali na nchi kwa ujumla imo katika mabadiliko makubwa hivyo ni lazima watambue wao ni sehemu ya mchakato huo katika kufanikisha masuala ya kisheria.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi hicho Mkurugenzi msaidizi wa idara ya huduma za sheria ofisi ya Rais TAMISEMI Eustard Ngatale amesema wanahitaji kuomba miongozo mbalimbali iliyowasilishwa kwao ikamilike haraka ili waweze kuitumia katika utekelezaji wa majukumu.

“Kwanza nimshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuandaa mkutano huu lakini pia nipende kuomba miongozo iliyowasilishwa kwetu ikamilike haraka ili tuweze kuitumia katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku,” amesema Ngatale.

Katika mkutano huo rasimu ya miongozo iliyowasilishwa kwa wanasheria hao ni pamoja na ule wa kutunga sheria ndogo, upekuzi wa mikataba mbalimbali, majadiliano ya mikataba yote, usimamizi wa utekelezaji wa Mikataba na muongozo wa utoaji wa ushauri wa kisheria.

Video: Fella aandika waraka mzito kwa Mbosso kuhusu kujitoa WCB
Neymar asababisha wachezaji Barcelona kucheleweshwa mishahara yao