Jeshi la Polisi nchini limesema Operesheni ya kukabiliana na mtandao wa dawa za kulevya katika Visiwa vya Zanzibar itaendelea sambamba na kuwadhibiti wahalifu wanaofanya vitendo vya kuwaibia na kuwadhuru watalii jambo ambalo linatia doa usalama uliopo katika visiwa hivyo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Operesheni maalum za Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Liberatus Sabas ambaye yupo Zanzibar akiongoza timu iliyoundwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini pamoja na Kamisheni ya Polisi Zanzibar kwa lengo la kuongeza nguvu katika kuzuia na kupambana na mtandao wa dawa za kulevya pamoja na uhalifu dhidi ya watalii.

DCP Sabas amesema Operesheni hiyo haitawaacha wahalifu hao salama kwa kuwa inafanyika kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kuwa haiachi mhalifu yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo viovu ambavyo vimekuwa vikichafua taswira nzuri ya usalama.

“Operesheni hii ni endelevu na niwape tu salamu wahalifu kuwa jambo la msingi ni wao wenyewe kujisalimisha kwa kuwa awamu hii hata wakikimbia tutawasaka na kuwakamata kwa kuwa nguvu ipo na tunapata ushirikiano kwa wananchi wema wanaochukia vitendo vya uhalifu” Alisema Sabas.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kamishna Msaidizi wa Polisi Hasina Tawfiqi amesema katika operesheni hiyo wamefanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya Heroin jumla ya Kete 695 sawa na ujazo wa gramu 31.3 pamoja na Watuhumiwa 21.

Amewasihii wakazi wa Kaskazini Unguja na mikoa jirani kuendelea kutoa taarifa ili kuweza kukomesha mtandao wa biashara hiyo pamoja na kuhakikisha kuwa watalii wanaotembelea mkoa huo wanafanya kazi zao
kwa amani na usalama.

Operesheni hiyo pia imefanyika katika Mkoa wa Mjini magharibi ambapo Jumla ya watuhumiwa 58 walikamatwa pamoja na dawa za kulevya aina heroin Kete 1293 na Vifuko vitatu sawa na Gramu 74.385.

Video: DataVision yatoa maelfu ya ajira, yaibua vipaji
TFF yazidi kumwanika Wambura