Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma linawashikilia watu sita wanne wakiwa ni raia wa nchi za Somalia na Ethiopia kwa kuingia nchini bila kibali sambamba na Watanzania wawili waliokuwa wakiwasafirisha wahamiaji hao haramu.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amesema watu hao walikamatwa Oktoba 23, 2019 katika kijiji na kata ya Mtera kilochopo tarafa ya Rudi Wilayani Mpwapwa.

Amewataja waliokamatwa kuwa ni Sellamu Yohanes (24) na Ashetu Tesfaye (20) wote wakiwa ni raia wa Ethiopia, Mahamoud Mapaa (19) na Cuse Ciise (18) raia wa Somalia na Watanzania Jamali Babuu Martin (26) na Makia Ally (25) ambao ni madereva wa bodaboda.

“Mbinu waliyoitumia watuhimiwa ni kuingia nchini kwa kutumia usafiri wa pikipiki mbili kuvuka mipaka na vizuizi vya barabarani na walikuwa na pikipiki aina ya Kinglion yenye namba za usajili MC 942 AXK na Dayun yenye namba za usajili MC 767 CEB,” amefafanua Muroto.

Aidha Kamanda Muroto amebainisha kuwa watuhumiwa walijaribu kuwarubuni askari waliowakamata kwa kutoa rushwa ya Tsh. milioni moja ili waweze kuwaachia lakini askari walikataa na kuwafikisha kituoni na wanatarajia kufikishwa Mahakamani.

Katika tukio jingine Kamanda Moroto amesema Polisi inawashikilia watu wawili kwa kukutwa na nyara za Serikali ambayo ni pembe moja ya jino la Tembo walilokuwa wamelihifadhi ndani ya kiroba kinyume cha sheria.

Amesema tukio hilo limetokea Oktoba 21, 2019 katika kijiji na kata ya Mkoka iliyopo tarafa ya Zoisa Wilayani Kongwa kwa kuwahusisha Stephano Mtagwa Kogani (39) na Hamis Mathayo Mabuku (45) ambao wanatarajia kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

“Kuna tukio jingine la kuvunja nyumba mchana na kuiba ambapo tumemkamata Elias Shaban Joseph (21) mkazi wa Mailimbili Mnadani baada ya kuvunja nyumba na kuiba maboksi 8 ya mafuta ya kupaka na maboksi 4 ya pipi yenye thamani ya shilingi 720,000 mali ya Willy Fidelis Mgeni,” ameongeza Kamanda Muroto.

Kufuatia matukio hayo Kamanda Muroto amesema wananchi hawana budi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeahi la Polisi ili kuzuia na kukomesha uhalifu huku akivipongeza vyombo vya habari kwa juhudi za dhati za kuihabarisha jamii.

Video: Ukweli juu ya sheria ya Ndoa, Njia za kuoa, umri chini ya miaka 18
Zari ahama nyumba aliyozawadiwa na Diamond, atangaza ndoa hivi karibuni