Jeshi la polisi nchini Canada jana lililazimika kuingilia kati msongamano wa watu kwenye maduka yaliyoanza kuuza bangi tangu alfajiri hadi usiku, kufuatia kupitishwa kwa sheria inayohalalisha matumizi ya mmea huo.

Wanunuzi walipanga foleni zilizodumu kwa zaidi ya saa 12, hali iliyofanya polisi kuingilia kati kutawanya umati wa watu majira ya usiku.

Baada ya kusubiri kwa takribani saa saba kwenye foleni, Alexandre mwenye umri wa miaka 30 alifanikiwa majira ya saa tatu usiku, dakika chache kabla ya polisi kuingilia kati na kufunga.

“Ilikuwa kazi ngumu kusubiri, kulikuwa na baridi kali. Lakini nimefurahi tu, kuzungumza na umati wa watu kwenye foleni hadi kununua bidhaa,” Reuters wanamkariri Alexandre.

Jana ilikuwa siku ya kihistoria kwa nchi hiyo, ikiwa ni nchi ya pili duniani baada ya Uruguay kupitisha sheria rasmi ya kuruhusu matumizi ya bangi.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya kampeni ya mwaka 2015 ya Waziri Mkuu, Justin Trudeau, ambaye alisema kuwa ataruhusu matumizi ya bangi kwa lengo la ‘kuwalinda vijana’ na kumaliza mtandao wa wauza dawa za kulevya.

Hata hivyo, hatua hiyo imekuwa ikipingwa na madaktari pamoja na upande wa vyama vya upinzani.

Serikali ya nchi hiyo imeeleza kuwa, takwimu zinaonesha takribani raia milioni 5.4 wa Canada watanunua bangi kwenye vituo vilivyopewa kibali maalum kwa ajili ya tiba mwaka 2018, ambao ni asilimia 15 ya idadi ya watu wote wa nchi hiyo.

Mahakama yapiga chini pingamizi la matokeo ya urais
Mwanafunzi ajifungua kwenye choo cha shule