Afisa wa Jeshi la Polisi wa Kaunti ya Narok nchini Kenya, anashikiliwa na vyombo vya dola nchini humo baada ya kunaswa akiwa katika nyumba ya kulala wageni (‘gesti’) na mwanafunzi wa kike wa shule ya Sekondari ya Sankale aliyekuwa anafanya mitihani ya kuhitimu.

Taarifa za jeshi la polisi zimemtaja afisa huyo kwa jina la Patrick Mwendo na kueleza kuwa alikamatwa Jumanne usiku baada ya kuwekewa mtego.

Kamishna Msaidizi wa Trans Mara, Mohammed Noor Hassan ameviambia vyombo vya habari kuwa walipata taarifa mapema kuwa mtuhumiwa huyo amechukua chumba katika nyumba ya kulala wageni na kwamba anatarajia kuingia na mwanafunzi.

Ameeleza kuwa walisubiri hadi usiku na walifanikiwa kumuona akiingia na mwanafunzi huyo kisha kuwatia nguvuni wote wawili.

Hassan amesema wanawashikilia Patrick na mwanafunzi huyo na kwamba wanaendelea kufanya utaratibu ili mwanafunzi huyo aendelee kufanya mitihani yake wakati uchunguzi ukiendelea.

Aidha, Hassan ameongeza kuwa mmiliki wa nyumba hiyo ya wageni amenyang’anywa leseni yake ya biashara kwa kosa la kumrusu msichana huyo kuingia ndani ya vyumba na mtu mzima.

Aliwataka wananchi kwa ujumla kushirikiana katika kuhakikisha mimba za utotoni zinadhibitiwa ipasavyo.

FA awaombea msamaha WCB, Basata wampa masharti
Video: Mabinti Nillah, Tannah waamua 'KUSEMA' ukweli kuiokoa jamii

Comments

comments