Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, amesema kuwa ubaguzi ndio chanzo kikubwa cha kushindwa mara mbili mfululizo katika uchaguzi wa Jimbo la Mbeya Mjini linaloongozwa na Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM ngazi mbalimbali wa Wilaya ya Mbeya Mjini, ambapo amefafanua kwamba siasa za makundi na ubaguzi wa kikabila zimekuwa zikiikosesha CCM ushindi kwenye jimbo hilo la Mbeya.

Amesema kuwa tatizo hilo lilibainika wakati uongozi wa juu ulipofanya tathmini ya majimbo ambayo CCM haikushinda kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, likiwemo jimbo hilo ambalo ni ngome ya CHADEMA.

Aidha, ameongeza kuwa ubaguzi huo umekuwa ukiifanya CCM kuonekana dhaifu mbele ya wapinzani na hivyo kukosa hoja kwenye uchaguzi pamoja na kuwapa faida wapinzani.

“Siasa za ubaguzi wa kikabila haziwezi kutufikisha popote, haijalishi kiongozi huyo anatoka kabila gani, cha msingi awe anashughulikia changamoto za wananchi. Viongozi fanyeni kila linalowezekana kuondoa tatizo hilo, ili tushinde kwenye chaguzi zijazo,“amesema Polepole

Hata hivyo, Polepole ameongeza kuwa ubaguzi wa aina hiyo ni wa miaka mingi hivyo akawataka viongozi wa chama hicho kuhakikisha wanaondoa changamoto hiyo haraka, ili kufanikisha ushindi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani na Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Video: Ukiwa Mjane watu wanakukimbia- Salome Komba
Raia wa kigeni akwepa jela alipishwa mamilioni