Huenda wachezaji Paul Pogba na Bruno Fernandes wakaukosa mchezo wa Ligi ya England (EPL) kati ya Manchester United dhidi ya Bournemouth baada ya ripoti kusema kuwa jana waliumia mazoezini.

Kwa mujibu wa mtandao wa The Mirror, inaelezwa kuwa wawili hao waligongana wenyewe kwa wenyewe na Fernandes ndiye aliyeonekana kuumia zaidi. Tukio hilo lilitokea wakati United ilipokuwa inapasha kwenye Uwanja wake wa mazoezi, Carrington.

Majeraha ya wawili hao yanaweza kuwa pigo kwa Meneja wa Mann Utd, Ole Gunnar Solskjaer kutokana na mchango mkubwa ambao nyota hao wawili wamekuwa wakiutoa kwa timu.

Pogba na  Fernandes wamekuwa na maelewano mazuri tangu walipoanza kucheza pamoja katika michezo ya hivi karibuni hivyo walibeba matumaini ya Manchester  United kumaliza katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi ya England.

Kwa namna inavyoelezwa huenda wachezaji hao wote au mmoja wao (Fernandes), akakosekana katika mchezo wa leo, kwani  walienda kufanyiwa matibabu baada ya kupata majeraha na kushindwa kuendelea na mazoezi.

Fernandes amekuwa na mchango mkubwa tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Sporting Lisbon ya Ureno katika dirisha la usajili la  Januari, 2020.

Amefunga  mabao sita na kutoa assisti nne katika michezo 13 aliyokichezea kikosi cha Ole Gunnar Solskjaer.

Kiungo huyo, amekuwa chachu ya mabadiliko kwa Manchester United ambayo kwa sasa wanacheza soka la kuvutia.

Vile vile Pogba, ambaye hakuwa na mwanzo mzuri wa msimu kutokana na kusumbuliwa na majeraha, alionekana kurejea akiwa katika ubora wake.

Manchester United wapo nafasi  ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu England wakiwa na pointi  52, wanapigania nafasi ya kumaliza katika nafasi nne za juu katika msimamo ili msimu ujao washiriki Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

Simba SC watangaza njaa Mtwara
FBI wanavyomnyoosha ‘Hushpuppi’, mwizi nguli mtandaoni