Kocha mkuu wa klabu ya Simba, Pierre Lechantre amesema kuna haja ya kufanya mabadiliko katyika kikosi chake itakapofika mwishoni mwa msimu huu, ili kuiboresha timu yake ambayo kwa sasa inaongoza msimamo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Lechantre amesema amekitazama kikosi chake na kufanya tathmini ya kina na baadae atakuja majawabu ya kuifumua Simba, na baadhi ya wachezaji atawapa mkono wa kwaheri.

Kocha huyo ambaye timu yake imetolewa kwenye Kombe la Shirikisho na Al Masry juzi usiku, alisisitiza msimu huu ukimalizika tu, lazima akifumue kikosi na kuvuta nyota wapya sita kwa mpigo ili kukifanya kitikise michuano ya kimataifa.

Lechantre anaonekana kuna kitu anaona kinamisi Simba, akasema anaona wachezaji kama John Bocco na Emmanuel Okwi, lakini tatizo ni kwamba kuna wengine ni kama mizigo kwa kushindwa kuisaidia timu hiyo.

Mfaransa huyo aliyewahi kuzinoa kwa mafanikio timu za taifa za Cameroon na DR Congo alisema kwa hali ilivyo anahitaji nyota wapya sita watakaoweza kuibadilisha timu na kuifanya iwe na makali ndani na nje ya nchi na si kuangalia Ligi Kuu pekee.

Alisema pamoja na maeneo mengine, watalazimika kuboresha safu yao ya kiungo pamoja na washambuliaji.

“Kwa ujumla tunahitaji wachezaji wenye uwezo wa kucheza mechi za ndani na hizi za kimataifa. Tukikosa kwenye Ligi ya ndani tutalazimika kutafuta wa kutoka nje,” alisisitiza.

Alisema Bocco na Okwi ambao wamefunga mabao 34 kwenye mashindano yote msimu huu, wanaitendea haki nafasi hiyo lakini tatizo ni kwamba hawana mbadala, endapo wawili hao wakikosekana kwa pamoja.

“Ukiwakosa Bocco na Okwi unachanganyikiwa, ukitazama kwenye timu hakuna mchezaji mwingine wa kukubeba. Hawa ni wachezaji hatari si tu hapa Tanzania, bali Afrika.

“Tunahitaji kuwa na wachezaji wengine wenye uwezo mkubwa kama wao au zaidi. Mavugo (Laudit) ni mzuri lakini tulipofika hapa hakuwa fiti hata kidogo, walau sasa tunamsaidia,” alisema Lechantre.

Kwa upande wa kiungo alisema waliopo sasa wengi sasa wengi ni washambuliaji hivyo wanahitaji kupata viungo wengine wa kusaidia kukaba.

“Tunahitaji pia wachezaji wa kukaba zaidi. Tuna viungo wengi wazuri lakini kwenye kushambulia. Wengi wakipoteza mpira hawasaidii sana kwenye kukaba, hiyo ndiyo sababu wakati mwingine tunalazimika kumtoa James Kotei kwenye beki na kumpanga kiungo,” alisema Lechantre.

Cristiano Ronaldo mchezaji bora Ureno
Azam Media wamalizana na Young Africans