Klabu ya West Ham United imeendelea kuiboresha safu yake ya ulinzi kwa kumsajili mlinda mlango kutoka nchini Poland Lukasz Fabianski, kwa mkataba wa miaka mitatu.

Lukasz Fabianski anajiunga na West Ham Utd akitokea klabu ya Swansea City ambayo msimu ujao itashiriki ligi daraja la kwanza, baada ya kushuka daraja ikitokea ligi kuu msimu wa 2017-18.

Usajili wa wachezaji wanaocheza katika safu ya ulinzi umenogeshwa na ujio wa meneja Manuel Pellegrini ambaye mwezi uliopita alitangazwa kuchukua nafasi ya David Moyes, aliyeondoka klabuni hapo.

Mapema hii leo West Ham Utd walitangaza kukamilisha usajili wa beki kutoka nchini Ufaransa Issa Diop akitokea klabu ya Toulouse inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Ufaransa (Ligue 1).

Fabianski mwenye umri 33, anaondoka Swansea City baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa misimu minne, na kwa bahati mbaya msimu uliopita aliruhusu kufungwa mabao 68 ambayo yalichangia kushuka daraja kwa klabu hiyo.

Kwa sasa mlinda mlango huyo wa zamani wa klabu ya Arsenal, yupo nchini Urusi, sambamba na kikosi cha timu ya taifa ya Poland ambacho jana kilishindwa kufurukuta mbele ya Senagal kwa kukubali kichapo cha mabao mawili kwa moja.

Fabianski ni chaguo la pili katika kikosi cha timu ya taifa ya Poland, akiongozwa na mlanda mlango Wojciech Szczesny wa klabu ya Juventus.

Mchezaji mwingine anaetajwa huenda akasajiliwa na klabu ya West Ham Utd baada ya Issa Diop na Fabianski, ni mlinda mlango Joe Hart, ambaye aliitumikia klabu hiyo kwa mkopo msimu uliopita akitokea kwa mabingwa wa soka nchini England Manchester City.

Mouez Hassen aondolewa kikosini
Marekani yajitoa UN yadai ni baraza la kinafiki