Gwiji wa soka kutoka nchini Ufaransa Patrick Vieira amesema anafurahishwa na hatua ya jina lake kujadiliwa na kuwa sehemu ya wanaofikiriwa kukabidhiwa jukumu la kukinoa kikosi cha Arsenal, baada ya kuondoka kwa Arsene Wenger.

Tangu Arsene Wenger alipotangaza kung’atuka mwishoni mwa msimu huu, jina la nahodha huyo wa zamani wa Arsenal limekua likitajwa kwa asilimia kubwa kupitia vyombo vya habari.

Vieira ambaye kwa sasa ni meneja wa klabu ya New York City FC inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini Marekani (MLS), amesema ni vizuri kusikia na kuona jina lake likihusishwa na mpango huo.

Amesema anaamini umahiri na utendaji mzuri wa kazi zake tangu alipoanza kuwa mkuu wa benchi la ufundi la New York City FC mwaka 2016, ni sababu kubwa ya jambo hilo kujitokeza kwa sasa.

Hata hivyo gwiji huyo amesema endapo ndoto ya jina lake kutajwa kuwa mrithi wa Arsene Wenger itatimia, atajihisi faraja kutokana na kuwa na mapenzi ya dhati na klabu ya Arsenal ambayo aliitumikia kwa mafanikio makubwa.

“Najua kuhusu jina langu kutajwa kila kukicha katika vyombo vya habari, inanifurahishwa kwa sababu ninaipenda kazi yangu na pia ninaipenda klabu ya Arsenal ambayo niliitumikia kwa moyo wangu wote.

“Wakati mwingine watu wanaweza kukukumbuka kutokana na mazuri uliowatendea, ninaamini niliondoka Arsenal kwa wema na kazi yangu niliyoifanya katika himaya ya klabu hiyo inaendelea kukumbukwa.” Amesema Vieira.

Viera anakumbukwa na wadau wengi wa soka duniani kufuatia uwezo wake mkubwa wa soka aliouonyesha katika kipindi chote alichoitumikia Arsenal kuanzia mwaka 1996–2005.

Patrick Vieira and Arsene WengerPatrick Vieira akiwa na Arsene Wenger mwaka 2004 katika sherehe za kutembeza kombe la ubingwa wa ligi ya England mitaa ya jijini London.

Viera alikua nahodha wa mwisho wa Arsenal kukabidhiwa kombe la ubingwa wa ligi ya nchini England, baada ya kikosi cha Arsene Wenger kumaliza msimu wa 2003/04 bila kupoteza mchezo hata mmoja wa ligi.

Chadema yapeleka ombi polisi
Video: LHRC yazindua ripoti ya Wasiojulikana