Huenda klabu ya Simba ikamkosa kocha wake Patrick Aussems baada ya kusadikika kuwa uongozi wa klabu ya Nkana ya nchini Zambia, umepanga kumpa mkataba mbeligiji huyo  kufuatia kuwepo kwa mchakato wa kuachana na kocha wao, Besto Chambesh.

Nkana wameanza mchakato huo kutokana na kocha wao kupewa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 23 itakayokwenda kushiriki michuano ya kombe la Mataifa Afrika (AFCON) itakayofanyika mwezi ujao nchini Misri.

Inadaiwa kamati ya ufundi ya timu hiyo, mpaka sasa imeshapendekeza majina ya makocha watatu ambao ni Aussems, Perry Mutapa wa Forest Rangers ya Zambia na CK Akounor aliyekuwa kocha wa Asante Kotoko ya Ghana.

“Huku Zambia hizo taarifa za Nkana kumtaka kocha wa Simba zipo kwa sababu ni miongoni mwa makocha watatu ambao wanawatupia jicho kali kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Chambeshi ambaye atakuwa Misri na timu ya taifa ya vijana kama kocha mkuu.

“Shida ni kwamba wenyewe wameamua kufanya jambo la siri, kwa kuwa bado lipo kwenye idara ya ufundi ambayo inatakiwa kumaliza mchakato lakini ukiangalia kwa upande wa kocha wa Simba, anapewa nafasi kubwa kutokana na rekodi yake CAF msimu uliopita,” kilisema chanzo kutoka nchini humo.

Mtendaji Mkuu wa Nkana, Charles Chakatazya ambaye amesema kuwa bado wapo na kocha wao mkuu hadi sasa na itakapofika muda wa kumtangaza kocha mpya watasema

“Bado tupo na Besto, hatuwezi kusema nani atakuja kwa sasa kwa kuwa hakuna kilichokamilika na hayo ni maneno kila mmoja anaongea lake lakini kwa sasa sisi tunaangalia zaidi timu na mwalimu ambaye yupo,” alisema Chakatazya.

Michuano ya Bashungwa Karagwe Cup yahitimishwa kwa kishindo
Mchezo wa Simba, Azam wapanguliwa