Pambano la wababe ambao hawajawahi kupigwa, Terrence Crawford wa Marekani na Jeff Horn wa Australia aliyemnyang’anya mkanda Manny Pacquiao, limeahirishwa huku wakiraruana kwenye vyombo vya habari.

Promota wa pambano hilo, Bob Arum ametangaza kuahirisha pambano hilo lililokuwa likisubiriwa kwa hamu Aprili 14 baada ya timu ya Crawford kuripoti kuwa mbabe huyo amepata majeraha mkononi.

Bob amesema kuwa kutokana na hali hiyo, pambano hilo litafanyika kati ya Mei au Juni mwaka huu.

Hata hivyo, Horn na timu yake wameelezea taarifa hiyo ya kuumia mkono kama dalili za uoga.

“Hawa mashabiki wote wa Marekani na wengine wanaosema kuwa Terence ni bondia mkali. Sasa kwanini asijitokeze apambane na mkono mmoja basi? Mimi nachukulia hii taarifa yao kama wameniogopa,” alisema Horn kwenye mkutano na waandishi wa habari nchini kwake.

Wakufunzi wa Horn walienda mbali zaidi yake wakimpaka matope Crawford kuwa amefanya tendo la kiuoga na kwamba hata akiahirisha, siku atakayopanda ulingoni atafunzwa adabu.

Naye Crawford ambaye anatajwa kuwa kati ya mabondia wakali zaidi Marekani kwa sasa, alitumia mtandao wa Twitter kumrarua moja kwa moja Horn akimtumia ujumbe kwa kumtaja (kum-mention) akiahidi kumkata ngebe.

“We endelea kufanya mazoezi na kuupa joto mkanda wangu wa ubingwa kwa sababu nitakufumua usiku wa pambano. Wewe, mimi na kila mmoja anajua hilo,” tafsiri isiyo rasmi ya tweet ya Crawford ambayo ilijaa pia maneno ya ukakasi.

Crawford ameshinda mapambano yake yote 32 na kati ya hayo 23 ni kwa kuwazimisha wapinzani wake kabla ya kengele ya mwisho (KO).

Naye Horn ameshinda mapambano 18 na kutoa sare ya pambano moja bila kupoteza.

Waziri Mkuu aamua kujiengua
Video: Lissu amvaa JPM, Vigogo watano TPDC kizimbani