Bondia Mfilipino Manny Pacquiao ametetea ubingwa wa dunia uzito wa Welterweight wa WBA dakika chache zilizopita, akimpiga kwa kumnyanyasa Adrien Broner.

Majaji wa pambano hilo lililoshuhudiwa Las Vegas nchini Marekani mbele ya mashabiki zaidi ya 13,000 wamempa ushindi wa raundi 8 kati ya raundi 12 (117-111, 116-112 and 116-112).

Vyombo vingine vya habari vilivyokuwa vinafuatilia vimetoa matokeo yake yasiyo rasmi. The Guardian imempa Pacquiao ushindi wa raundi 11 kati ya 12 (119-109) na CBS sports wamempa Pacquiao ushindi wa raundi 10 kati ya 12.

Manny Pacquiao baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa pambano kati yake na Adrien Broner

Katika pambano hilo, Bondia huyo Mfilipino ambaye pia ni Seneta nchini kwake aliwashangaza wengi kwa namna alivyotawala pambano dhidi ya kijana huyo machachari, kiasi cha kumfanya George Foreman, bondia gwiji anayekumbukwa kwa kupigana na Muhammad Ali nchini Zaire (Rumble in the Jungle) kumvulia kofia.

“Pac anaweza kuwa bondia mwenye umri wa miaka 40 aliye vizuri kuliko yeyote niliyemuona mwaka huu. Raundi 12 na harudi nyuma,” tafsiri ya tweet ya George Foreman.


Naye Lennox Lewis, bingwa wa zamani wa masumbwi ya uzito wa juu, alieleza kuwa, “ingawa Broner alikuwa na kasi, Manny Pacquiao mwenye umri wa miaka 40 alikuwa na kasi zaidi.”

Broner ana umri wa miaka 29 na amewahi kuwa bingwa wa dunia mara nne katika uzito tofauti tofauti.

Hata hivyo, mashabiki wamempongeza Broner kwa jinsi alivyoweza kuvumilia adhabu ya kipigo mfululizo kutoka kwa Pacquiao wakati wengi walitegemea asingemaliza raundi zote hususan baada ya kushuhudia raundi ya 7.

Hata hivyo, Broner amewashangaza wengi baada ya pambano hilo, baada ya kudai kuwa yeye ndiye mshindi na kwamba Pacquiao amepewa ushindi kwa sababu wanataka kutengeneza pesa ya pambano la marudiano kati yake na Mayweather.

Ushindi huu sasa unawapa hamasa zaidi mashabiki kutaka kulitazama pambano la marudiano kati ya Pacquiao na Mayweather, pambano ambalo litakuwa lingine kubwa zaidi katika historia ya masumbwi tangu wapande ulingoni Mei 2015, ambapo Mayweather alishinda.

“Mwambieni Floyd arudi ulingoni halafu tutapigana,” alisema Pacquiao baada ya pambano hilo. “Nina nia ya kupigana naye tena, kupigana na Floyd Mayweather,” aliongeza.

Ajira 5 zenye msongo wa mawazo zaidi duniani
Waandishi 38, wanaharakati kukamatwa kwa uchochezi mtandaoni