Mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona wameendelea kuhusishwa na mpango wa kuwa tayari kumuuza mshambuliaji wao wa pembeni kutoka nchini Ufaransa Ousmane Dembele, utakapofika wakati wa dirisha dogo la usajili (Januari  2019).

Vyombo vya habari vya Hispania vimedai kuwa, uongozi wa Barca upo tayari kufikia maamuzi ya kumuweka sokoni mshambuliaji huyo, kufuatia kuchoshwa na utovu wa nidhamu ambao kila leo amekua akiuonyesha klabuni hapo.

Inadaiwa Dembele amekua anashindwa kubadilika kila anapopewa nafasi, jambo ambalo limemfanya meneja wa Barca Ernesto Valverde, kuwasilisha mapendekezo ya kutaka mshambuliaji huyo auzwe mwezi Januari.

Taarifa zilizotolewa na vyombo hivyo vya habari zinaeleza kuwa, Dembele amekua hafiki kwa wakati mazoezini na amekua na uhusiano hafifu na wachezaji wenzake, jambo ambalo limeanza kuzua taharuki klabuni hapo.

Endapo Barca wakifanikisha mpango wa kumuweka sokoni mshambuliaji huyo wa zamani wa Borussia Dortmund ya Ujerumani, huenda thamani yake ikafikia Euro milioni 100.

Dembele alijiunga na Barcelona mwanzoni mwa msimu wa 2017/18 kwa ada ya uhamisho wa Euro milioni 105, na mpaka sasa ameshacheza michezo 28 na kufunga mabao saba.

Tayari klabu za Liverpool ya England na mabingwa wa soka nchini Ufaransa PSG wanatajwa kuwa katika harakati za kumuwania mshambuliaji huyo mwenye umriwa miaka 21.

Uwepo wa aliyekua meneja wa Borussia Dortmund  Thomas Tuchel kwenye kikosi cha PSG, unatajwa kuwa kichocheo kikubwa cha kushawishi usajili wa Dembele itakapofikia Januari 2019, endapo atawekwa sokoni.

AS Roma, AC Milan kupigana vikumbo usajili wa Benatia
#HapoKale