Serikali imesema kuwa itaendelea na juhudi za kushawishi wadau wa maendeleo na Jumuiya za Kimataifa ili kupata fedha za kusimamia uratibu wa shughuli za mazingira na kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi nchini.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba wakati wa kuwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira.

Makamba ameainisha mafanikio yaliyopatikana katika Ofisi yake kwa kipindi cha mwaka 2018/2019, kuwa ni pamoja na kufanya Mapitio ya Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997 na Mkakati wa Utekelezaji wake, kuandaa rasimu ya Mpango wa Taifa wa Mazingira wa mwaka 2019 – 2023, na Maandalizi ya Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Viumbe Vamizi (Invasive Alien Species).

Aidha, katika kipindi cha mwaka 2018/19, Ofisi ya Makamu wa Rais imekamilisha rasimu ya mwisho ya Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira nchini baada ya kupata maoni ya wadau kabla ya kuwasilishwa Bungeni kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004.

Pia, ameongeza kuwa katika kuhakikisha usimamizi na utekelezaji wa Sheria ya Mazingira unazingatiwa, jumla ya miradi 1,254 ya maendeleo imefanyiwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na Ukaguzi wa Mazingira ili kuharakisha uwekezaji katika sekta ya viwanda nchini, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira linatoa Kibali cha Awali cha Mazingira (Provisional Environmental Clearance) ili kuwawezesha wawekezaji kuendelea na maandalizi ya awali ya mradi wakati mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira unaendelea.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Suleiman Sadick amepongeza uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa jitihada za kuhifadhi mazingira nchini.

Tatizo la Maji Chalinze lapatiwa ufumbuzi
Msiponilipa mshahara wangu nawashtaki- Lissu

Comments

comments