Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema kuwa Serikali ipo macho masaa 24 katika siku 7 za wiki na itaendelea kuwabaini kuwakamata na kuwatia hatiani watoroshaji wa madini sambamba na kulinda rasilimali hizo.

Akizungumza katika Kongamano baina ya Wadau wa Madini lililoandaliwa na Tume ya Madini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) katika Maonyesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam,

Nyongo amesema kuwa kitendo cha utoroshaji wa madini ni kosa kisheria na hivyo wafanyabiashara wote wanatakiwa kufuata utaratibu uliowekwa na Serikali.

Kwa mujibu wa Waziri Nyongo katika mwaka wa fedha 2018/19 Serikali kupitia Tume ya Madini imevunja rekodi katika ukusanyaji wa mapato ya madini hatua iliyotokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano.

“Tangu uhuru nchi yetu haikuwahi kukusanya kiasi kikubwa cha fedha ambacho ni mapato yatokanayo na madini ya kiasi cha Tsh. Bilioni 310, hivyo Serikali itaendelea kuweka mkazo kuzuia njia za panya ambazo zimekuwa zikitumiwa na watoroshaji wa madini,”amesema Nyongo

Aidha, Nyongo amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali kupitia Tume ya Madini imepanga kukusanya kiasi cha Tsh. Bilioni 470 na hivyo amewataka watendaji wa Tume hiyo kuhakikisha kuwa malengo hayo yanafikiwa kwa kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu ikiwemo kuendelea kuwafichua na kuwakamata Wafanyabiashara wasiotaka kufuata sheria.

Hata hivyo, ameongeza kuwa Serikali kupitia Tume ya Madini kamwe haitamwonea mfanyabiashara yeyote anayefanya biashara zake kwa kufuata sheria ikiwemo kuuza madini yake katika masoko yaliyofunguliwa na Serikali kwani kwa kufanya hivyo kutawezesha Serikali kukusanya kodi yake pamoja na kuweza kuongeza mapato ya serikali.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE Zanzibar, Latifa Hamisi amesema kuwa Ofisi yake itaendelea kuimarisha ushiriakiano na wadau wote wa sekta ya biashara nchini ikiwemo wadau wa madini kwa kuwajengea uwezo sambamba na kuwafutia masoko ya uhakika wa bidhaa zao ndani na nje ya nchi.

Naye Rais wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Madini Nchini (FEMATA) John Bina ameiomba TANTRADE kuweka utaratibu wa kuwatembelea wachimbaji wadogo wa madini katika maeneo mbalimbali nchini ili kuweza kuzitambua changamoto zao kwa kuwa kupitia utaratibu huo utawawezesha kutambua mchango wao katika uzalishaji wa madini na nafasi waliyonayo katika kukuza uchumi wa nchi.

Video: TBA yaja na utaratibu mpya wa malipo
JPM atuma salamu za rambirambi Azam Media Limited