Kundi la Young Money  limetangaza kutoshiriki tena Tuzo za BET pamoja na kutumbuiza katika onesho la BET Experience mwaka huu, baada ya kuchukizwa na ujumbe wa kumsifu Cardi B ulioonesha dharau kwa mwanafamilia wao, Nicki Minaj.

BET waliweka kwenye mitandao ya kijamii pamoja na tovuti yao ujumbe wa kumpongeza Cardi B kwa kunyakua tuzo ya Albam Bora kwenye Tuzo za Grammy mwaka huu, kupitia kupitia albam yake ‘Invasion of Privacy’. Cardi B aliweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kushinda tuzo ya Albam Bora kama msanii pekee (solo), lakini sifa zilienda mbali na kumrushia tope hasimu mshindani wake, Nicki Minaj.

Sehemu ya ujumbe huo wa BET ilisomeka, “wakati huu, Nicki Minaj anaburuzwa na wigi lake (lacefront).” Ujumbe huo ambao hata hivyo uliondolewa baadaye, ulionesha kumkwaza Nicki ambaye alionesha hasira na kuanza kuretweet jumbe za mashabiki walioishambulia BET.

“Badala ya kuelezea mambo makubwa aliyoyafanya Nicki Minaj hadi kukwea ngazi kama mwanamke mweusi na kumhamasisha Cardi B kupata tuzo ya Grammy, au hata mtempongeza tu Cardi B; nyie kama chombo cha habari cha watu weusi mmeamua kuwaharibia wanawake weusi. Huu ni upuuzi kwa kuzingatia kuwa huu ni mwezi wa historia ya watu weusi,” aliandika shabiki mmoja, na Nicki akaretweet.

Kabla ya kutagaza kutoshiriki matukio hayo muhimu ya BET, Nicki Minaj pamoja na Lil Wayne walikuwa miongoni mwa wasanii ambao wamepangwa kutumbuiza kwenye ‘BET Experience’.

Tuzo za BET zitashuhudiwa Juni mwaka huu, na Cardi B anatarajiwa kuwa miongoni mwa watumbuizaji watakaoongoza hasa baada ya Nicki kujiondoa.

Hata hivyo, leo BET wameomba radhi kwa Nicki, Young Money na mashabiki wao kutokana na ujumbe huo. Wameeleza kuwa wanampena Nicki na kwamba ujumbe huo ulikosewa kwani wanaamini msanii huyo amefanya kazi kubwa ya kusaidia kuwahamasisha wasanii wengi.

“BET tunampenda Nicki Minaj. Tumekuwa tunamuunga mkono tangu alipoanza muziki na tutaendelea kwa jinsi anavyozidi kwenda mbele. Nicki ametengeneza njia kwa wasanii wengi na ametengeneza jina lake kama mmoja kati ya watu wenye nguvu kubwa kwenye kiwanda cha muziki,” wameandika BET.

Serikali yaweka mazingira mazuri ya uwekezaji
Serikali yabaini pipi, vidonge vyenye dawa mpya za kulevya

Comments

comments