Aliyekuwa mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari amesimulia jinsi alivyokuwa akimuuguza mke wake kutokana na matatizo aliyokuwa nayo na kusema alijaaliwa kupata mtoto wa kike Januari 27, siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano wa Bunge la Januari.

Nassari amesema hayo leo Jumapili Machi 17, 2019 wakati akizungumza na waandishi wa habari, siku chache baada ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kutangaza kwamba mbunge huyo hana sifa za kuendelea na ubunge.

Amesema kuwa mara ya mwisho alihudhuria mkutano wa Bunge wa Septemba lakini hakuhudhuria mkutano wa Novemba na Januari kwa sababu alikuwa anamuuguza mke wake huko Marekani.

Amesema alikuwa njia panda kuamua kati ya kuhudhuria vikao vya Bunge au kukaa na mke wake ambaye alikuwa mgonjwa.

“Nilifanya jitihada za kuwasiliana na Spika, nikamtumia ‘email’ (barua pepe) nikiwa Marekani kumjulisha hali ya mke wangu.” Amesema Nassari

Nassari amesema atakwenda Mahakamani kutafuta haki ya uwakilishi wa wananchi wa Arumeru, hata hivyo ameongeza kuwa Spika bado ana nafasi ya kurejea uamuzi wake ili wananchi wa Arumeru waendelee kuwa na mwakilishi katika Bunge.

“Nasikitika kwa uamuzi alioufanya, nawapa pole wananchi wangu wa Arumeru, haki yao tutaitafuta kwenye vyombo vya sheria,” ameongeza Nassari.

Amesema hajutii uamuzi wake wa kusimamia kiapo chake cha ndoa kwa kuamua kumuuguza mke wake.

“Bado nina furaha ya kupata mtoto, pamoja na huzuni ya kuvuliwa ubunge. Kuwa mbunge hakuondoi majukumu mengine ya kifamilia. Spika alihudhuria harusi yangu mwaka 2014, alikuwa anajua sina mtoto na nilimjulisha juu ya matatizo ya mke wangu.” amesema Nassari.

Machi 14, 2019, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amemuandika barua, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Semistocles Kaijage kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki kwa sasa liko wazi kufuatia, Mbunge wake Joshua Nassari (Chadema) kushindwa kuhudhuria mikutano mitatu mfululizo na hivyo kupoteza sifa za kuendelea kuwa Mbunge.

Mwanasheria ampiga risasi wakitoka kanisani
Ombi la Mbunge Msukuma kwa Waziri Mkuu, 'Yasijengwe masoko mengine mikoani'