Na Edward Lucas

Ukiona ndege ametua kwenye ulimbo, kanasa lakini hana wasiwasi, anachambua tu mbawa zake mithili ya mrembo aliye mbele ya dressing table, basi fahamu kuwa ndege huyo amegundua amenasa kwenye ulimbo uliotegwa bahati mbaya na ‘Rasta Man’ asiyekula nyama. Vinginevyo yatakuwa ‘mang’ana’.

Hebu fuatilia kilichonikuta, cha ajabu na cha kushangaza kilichoniuguza… ni mapenzi gani haya au uchawi, au ni wizi gani huu!!!

Juzi nilikuwa katika mizunguko yangu ya kila siku, ila ilipofika majira ya saa mbili usiku hivi ilibidi nielekee kituo cha daladala ili nirejee kwenye kiota changu. Nilikuwa na uchovu mwingi hata honi za daladala nilihisi zinanipigia kelele.

Kama unavyojua jiji la Dar es Salaam, adha ya usafiri ni kubwa. Licha ya kuwa na rundo la daladala, bado abiria wanafunika wingi wa daladala hizo. Kwahiyo panahitaji msuri wa maana kupata gari hasa majira ya jioni.

Bahat nzuri siku hiyo nimefika pale Mawasiliano (Simu 2000), daladala nayo ndo ikawa inaingia kwahiyo ikabidi niwahi haraka ili nipate seat, japo kwa uelekeo wetu watu sio wengi sana ila kwa kiasi fulani kulikuwa na kambanano kidogo. Lakini kwa muda huo upande wetu gari ilikuwa wazi kidogo, so nilifika nikapata seat nikakaa.

Nikiwa hata sijatulia vizuri alikuja dada fulani akiwa kasi sana kama alikuwa anawahi seat wakati gari bado ilikuwa na seat za kutosha! Alikuja hadi pale nilipokuwa nimekaa akanambia, “samaha ni sogea kidogo tukae wote”.  “Bila samahani dada, pita ukae upande wa dirishani,” nilimjibu kwa sababu ilikuwa seat ya watu wawili. Nilimpisha akakaa upande wa dirishani mkono wa kulia ule upande wa dereva

Lakini muda mfupi tu gari likiwa ndo linaanza kuondoka. Ghafla, nilimuona anatapatapa kuangalia kwenye mkoba. Mara ajikague kama anatafuta kitu. Baadae, nikamsikia anajisemesha kwa huruma, “mmmm simu yangu jamani” huku zoezi la kujipekuapekua likiendelea.

Mimi nilikuwa nimechoka, natamani hata kusinzia, nikaanza kuwaza, “sasa huu msala wa simu tena..”

Akiwa anafanya hayo nilikuwa nimetulia kama simuoni hivi wala simsikii… Sikuonesha ushirikiano wala kumsikiliza. Alishindwa kutulia, mara akanigeukia na kuniambia, “kaka samahani, unaweza kunibipia simu yangu hapo mara moja”. Basi mtoto wa watu hata sikuuliza kitu nilishika simu na akanitajia namba zake kisha nikapiga simu kwa ile namba.

Punde simu ilianza kuita ikiwa kwenye mkoba wake…, ni uleule mkoba aliokuwa anausachi. Hapo hapo akasema “heee afadhali kumbe iko humu!!!! nilikuwa nimeshaogopa… asante sana kaka.” Sikuwa na maneno mengi nikamjibu, “usijali.” Safari yetu ikaendelea huku yowe la konda la vituo likiendelea. Niliifuta ile namba palepale, najua fujo za mpenzi wangu akiishika simu yangu huko nyumbani halafu aone namba mpya ambayo sina maelezo yake.

Lakini kupitia hiyo “oparesheni saka simu”  nilipata nafasi ya kumuangalia vizuri usoni. Nilimuona binti mrembo halafu kama wa kishua sana. Nilihisi alipaki gari lake sehemu akapanda daladala. Lakini kwa udadisi wa jicho langu niliona kama tayari ameshazaa. Si ujaua tena jicho linatuma taarifa nyingi kwenye ubongo.

Pua zangu zilisia harufu nzuri ya marashi. Yaani ile seat ilikuwa na hali nzuri muda ule. Sio marashi makali, ni laini ila yanavutia, nikaanza kuhisi raha kwa mbali. Sio rahisi kuisikia ile harufu uswahilini kwetu.

Lakini cha ajabu kipindi kondakta anatangaza kituo kinachofuata yule dada aliomba ashushwe pale…nilishtuka kidogo maana ni karibu sana na pale tulipopandia yaani hata mtu akisamama anaweza kumuita mtu wa kituo cha pili. Kama unavyojua vituo vya town. Nikasema kimoyomoyo kikwetu, “bhono mbosari bhwa sihera”. Yaani huu ni uharibifu mkubwa wa fedha.

Aliposimama, kwa kweli jicho lilimuangalia kidogo… eeh, alikuwa amejaliwa, mwembamba hivi ila nyuma alikuwa na minofu. Basi, niliishia kumuangalia hadi mlangoni. Basi nikaendelea na mambo yangu. Nikawa nafikiria kwa mbali..”huyu vipi!?”

Baada ya kuwa ameshuka na safari imeendelea kondakta alianza kukusanya nauli na alianzia kwangu lakini baada ya kunipa chenji aliniuliza “huyo dada mnafahamiana?” “Dada yupi?” nikamuuiliza Konda. “Huyo aliyeshuka hapo” nikamwambia, “hapana!” Yule konda akaguna kama mtu anayetahadhalisha jambo.

Konda akaniuliza “kwani unashukia wapi” nikamwambia mwisho wa daladala, basi akasema ngoja achukue kwanza nauli kwa abiria kisha tuongee..Yale maneno yake yalinishtua kidogo ikabidi nianze kujikagua labda kuna kitu nimepoteza lakini sikuwa na kitu chochote nilichopoteza so ikabidi nimsubiri kwa hamu na maswali mengi sana kichwani.

Nikiwa nasubiri konda amalize kukusanya nauli ili anambie nini kinaendelea, mapigo ya moyo yalianza kwenda mbio kidogo nikijiuliza mambo mengi kuhusu huyo mtu. Kubwa likiwa nini nimepoteza. So niliendelea kujikaguakagua kwa kila nilichokuwa nafikiria lakini kwa kadIri nilivyojitathimini nilijiridhisha kuwa sijapoteza chochote hivyo ikabidi nisubiri maneno toka kwa kondakta.

Basi kondakta baada ya kumaliza kuchukua nauli alirudi kukaa kwenye kiti kilichokuwa mlangoni nami nilivyoona hivyo ikabidi nisogee siti ya mbele kidogo ili niwe karibu naye wakati huo baadhi ya siti zilikuwa wazi maana abiria wengi walikuwa wameshuka..kwahiyo nikakaa upande ule wa dereva yaani kulia mwa gari huku konda akiwa upande wa kushoto kule mlangoni.

Nilinyoosha mkono nikamgusa kondakta begani alipogeuka nikamwambia “hebu nambie mkuu, kuna nini?” Jamaa aligeuka na aliponiona ni mimi akasema “aaaaah!! nilikuwa nishasahau boss.”

Basi akaweka sarafu na noti zake vizuri kwenye koti na akaanza kunisimulia.

Kama unavyojua konda na mlango…so jamaa akanambia kipindi gari linafika katika kituo akiwa pale mlangoni , alimuona huyo dada akiwa na wenzake wawili wakiwa wamesimama miongoni mwa kundi kubwa la abiria. Waliokuwa pale kituoni ambapo licha ya baadhi ya abiria kukimbia kuja katika daladala hiyo wao walibakia wamesimama..jambo ambalo ni la kawaida tu. Akahisi sio gari walilokuwa wanasubiri.

Lakini ghafla mimi nikiwa nakimbia kuelekea katika hilo gari, Konda anasema aliwaona wanaoneshea kidole yaani mmoja kati yao alikuwa ananisontea kidole ishara ya kuwaonesha wenzie (nadhani hapo nitakuwa nimeeleweka vizuri) na hasa aliyekuwa anaelekezwa ni huyu aliyekuja kwenye gari.

Katika zoezi hilo ilionekana wale wengine wawili wanamshinikiza yule dada anifuate ambapo naye alionekana kusitasita. Nikiwa ndo ile naingia tu kwenye daladala hatimaye alipochomoka mbio kuja katika ile gari.

Hii movie yote kumbe yule kondakta aliiona….alianza kujiuliza kuwa pengine tunafahamiana lakini pia mawazo yake yalimtuma labda kuna jambo wanataka kulifanya kwangu. Kwahiyo, kwa kiasi fulani alianza kuweka kuangalia kwa makini hasa kwa yule mtu hata pale gari alipokuwa linaondoka.

Kumbe hata katika zile harakati za “oparesheni saka simu” kondakta alikuwa anatupimia tu ki-wiziwizi ili kama kutatokea shida yoyote basi aweze kubanana naye. Kumbe hata kile kitendo cha yule dada kushuka mapema ndo kilimshtua zaidi, akahisi kuna tukio lishafanyika tayari. Kwahiyo pale nje alimcheleweshea chenji kidogo ili kama kutasikika mtu analalamika humo ndani ya daladala basi aweze kumdandia lakini ilikuwa haina namna alimpa chenji na tukaendelea na safari.

Ndo maana aliporudi ndani ya gari tu akaanzia kwangu na kuniuliza kama nafahamiana naye. So, kondakta baada ya kunisimulia haya yote mwishoni tena alirudia kuniuliza swali lile lile “vipi wewe humfahamu kabisa?”

Nikamjibu, “hapana mzee wala sijawahi kumuona hata mara moja, ndo hivi leo tu”. Basi konda aliniuliza tena “vipi vitu vyako vyote viko sawa?” “Naona kila kitu kiko sawa.”

Basi aliyafunga mazungumzo yetu lakini maneno aliyomaliza nayo ndo yalinishtua sana, aliguna kisha akasema “inabidi uje ujichunguze vizuri maana huo ujio wake sio wa kawaida halafu siku hizi kuna vimambo vya ajabu ajabu huku, basi tu.” Basia akaendelea na kazi yake.

Daaaah!!!! Kusikia hili neno akili ilianza kufikiria maneno mengine mazito kidogo…yaani mbali na akili ya kupoteza kitu nilianza kujichunguza labda kuna kitu kisicho cha kawaida nimeachiwa au hata kupakwa. Lakini yule msichana mbona anaonekana wa kishua..!

Nilijitazama sana upande wa kulia maana alikuwa amekaa kulia kwangu. Lakini kila nilipotaza sikugundua kitu akili ikanituma nigeuke nyuma nitazame pale kwenye siti tulipokuwa tumekaa naye.

Lakini niliposimama tu kutazama kule kwenye siti..moyo ukashtuka mithili ya mvunjiko wa ‘bawaba’. Nikakumbuka wakati anatafuta simu yake aliniomba nimbeep…na baada ya kumbeep simu yake aliipata katika mkoba wake hivyo akili ikanituma haraka haraka labda shida kubwa ilikuwa ni mawasiliano yangu na ile njia ya kuvunga kapoteza simu ilikuwa ni gia tu ya kupata namba yangu.

Kweli nilijidharau kwa muda nikajiona mimi bata kweli..yaani mtoto wa kike kanizidi ujanja kiulaini namna hiyo!!. Basi nikaona haina shida nisubiri hicho kitakachojili na kama sio hivyo nilivyofikiri basi liwalo na liwe..kwa muda huo sikushtuka kuangalia namba yake katika simu yangu maana baada ya kuipata simu yake tu, namba yake niliifuta.

Baada ya daladala kufika kituoni nilishuka na kuanza kutembea mdogo mdogo kuelekea home huku njiani nikiwa natafakari nini dhima ya yule dada. Lakini nilipofika nyumbani wakati wa kuvua viatu na soksi ndo “nilistajabu ya Musa kabla sijaona ya Filauni”

Mwanzoni nilipoitazama niliona kama suluali yangu imedondokewa na vitu vyeupe mithili ya unga au poda katika mguu wa kulia karibu na viatu….ambapo nilitumia dekio la mlangoni kufuta uchafu huo na ukatoka kawaida lakini nilipokuwa najifuta, nilikuta suluali yangu imekatwa ka-kipande kadogo kiasi usawa wa pindo la suluali chini kabisa katika mguu wa kulia.

Nilianza kujiuliza ni wapi nilipopita hadi suluali yangu kuchafuka namna hiyo sikupata jibu lakini nilipo iona ile sehemu iliyochanwa na kuondolewa kabisa sehemu ya kipande cha suluali nilipatwa na hofu sana na akili ikanituma moja kwa moja kuwa hiyo ni kazi ya yule dada aliyekuwa katika daladala.

Ndipo nilipokumbuka muda flani nikiwa mle kwenye daladala muda mfupi baada ya kupata simu yake nilimuona akifungua mkoba na kutoa kitana, kioo na vitu vingine ambavyo sikuvichunguza vizuri kisha akainama kidogo katika seati akawa kama anaseti nywele si unajua tena mambo ya wanawake wa town.

Lakini katika harakati ile nilimsikia kama kadondosha kitu, halafu akainama chini kwenye siti kukiokota ambapo aliinamana kwa sekunde kadha kisha akainuka na kuchukua vitu vingine na kuvirejesha katika mkoba….mimi kwa wakati huo nilikuwa simzingatii sana tena nilikuwa namwangalia kiwiziwizi.

Ndipo nilipopata jibu kwamba muda huo ndo aliutumia kufanya kitendo hicho..lakini swali linabaki “nini haswa kusudi la kitendo hiki?” Na je, mimi nitaathilika kwa namna gani kuhusu hilo?.  “kwanini mimi?”. Maana ilionekana walisonteana kidole kisha mmoja akaniwahi katika gari…haya yote yanaendelea kunichanganya sana.

Lakini kila napofikiria na kusubiri kuona hicho kitakachotokea nikijiuliza nini tena matumizi ya namba yangu ambayo aliipata kiujanja ujanja.. “kweli sipati jibu”, kwa bahati mbaya mimi yake niliifuta ningeweza kumtafuta lakini pia kwa upande mwingine najipa matumaini kwamba kama alichukua namba basi atanitafuta….japo kwa nafasi hii nahisi labda ni kwa matumizi yake.

Nafikiria mambo mengi sana lakini sipati jibu kuwa ni ushirikiana wa kunidhuru, ni ushirikina wa kuweka mambo yake sawa? Au ndo nalogwa nidate kwenye mapenzi mazito ya mtoto wa kishua? Lakini kakosa nini hadi mimi.. tena kwenye daladala, hajawahi kuniona hata siku moja? Nguo yangu inahusikaje? Nimebaki na maswali sipati jibu, najuta kuifuta ile namba bora ningempigia mapema nimuulize.

Hapa sina jinsi zaidi ya kusubiri kitakachonikuta… ila hofu yenyewe inanikondesha kila kukicha na namuogopa kila ninaekaa naye kwenye daladala.. Nasubiri na bado sina jibu! Kilichobaki ni maombi tu.

TFF Yatuma Salamu Za Rambirambi Klabu Ya Tanzania Prisons
Wabunge wa Ukawa wagomea uteuzi wa Ndugai