Droo ya makundi ya michuano ya ligi ya Mabingwa barani Afrika pamoja na hatua ya mtoano ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, inatarajiwa kufanyika kesho Jumatano huku Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera akisema hana hofu pia yupo tayari kukutana na timu yoyote ile hata za kutoka kaskazini mwa bara la Afrika.

Kesho Yanga itapata kumjua mpinzani wake watakayekutana naye katika mchezo wa kusaka nafasi ya kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo na kwa mujibu wa ratiba ya Caf, mchezo wa kwanza utapigwa Oktoba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na marudiano ni Novemba 3, ugenini.

Zahera amesema kuwa soka la Afrika limebadilika hivi sasa, kwani viwango vya wachezaji vinafanana hali inayompa matumaini huku akiongeza kuwa amejifunza vitu vingi kuondolewa kwao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo amepanga kurekebisha makosa waliyoyafanya ili yasijitokeze katika shirikisho.

“Soka la Afrika hivi sasa limebadilika kwa kiwango kikubwa, awali timu nyingi zilikuwa zinazihofia timu za Waarabu, lakini hivi sasa hawaziogopi kutokana na ubora wao kupungua. Hivyo, mimi kama kocha nipo tayari kukutana na timu yoyote kutoka Uarabuni, na nina uhakika wa kupata matokeo mazuri nyumbani na ugenini,” alisema Zahera.

Miongoni mwa timu ambazo Yanga inaweza kupangwa nazo ni Paradou AC ya Algeria, ESAE ya Benin, DC Motema Pembe ya DRC na FC San Pedro ya Ivory Coast, Pyramids ya Misri, Bandari ya Kenya, Bidvest Wits ya Afrika Kusini, TS Galaxy ya Afrika Kusini, Proline ya Uganda na Triangle United ya Zimbabwe.

Droo hiyo inatarajiwa kupangwa jijini Cairo, Misri na Yanga inashiriki Kombe la Shirikisho baada ya kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Zesco United ya Zambia.

Fabian Delph aondolewa kikosini
Ulaji chakula kupitiliza husababisha Saratani