Mwili wa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha usafirishaji (NIT),  Akwilina Akwiline umepokelewa Hospitali ya Taifa Muhimbili MNH leo jumatatu.

Mwili huo umehamishiwa Muhimbili ukitokea Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

Ndugu wa marehemu wamekusanyika Muhimbili katika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti, wakisubiri uchunguzi ukamilike ili kujua hatma ya kuusafirisha kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika wiliyani Rombo mkoani Kilimanjaro.

Kaka wa marehemu, Moses Kiyeyeu amesema madaktari na wahusika wengine wanaendelea na utaratibu wa uchunguzi wa mwili.

”Mwili umefikishwa hapa tangu asubuhi na kule ndani kuna kaka yetu ndiye anashuhudia uchunguzi huo, wametwambia tutoke kwanza ndani watatuita baadaye ili kupewa taarifa nini kinafuata kuhusu mwili wa ndugu yetu” amesema kaka mtu.

Akwilina amefariki dunia Februari 16, 2018 baada ya kupigwa risasi kichwani akiwa kwenye daladala na polisi walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa Chadema.

Wanafunzi wapanga maandamano kupinga mashambulio
Gari la msafara wa Rais Kabila lapata ajali, laua