Mwenyekiti wa CCM tawi la Ubaruku, Ally Mazinge (66), ameuawa kwa kukatwa na shoka kichwani usiku, wakati akiwa amelala na familia yake nyumbani kwake.

Imeelezwa kuwa tukio hilo limetokea wilayani Mbarali mkoani Mbeya, Juni 27 saa 6:30 usiku baada ya mke wa marahemu kwenda kujisaidia usiku huo licha ya kuwa umbali wa choo na nyumba sio mrefu.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mbuyuni, Francis Mayemba ameliambia gazeti la mwananchi kuwa alitoa taarifa ya kifo hicho polisi, ambao walifika na kuangalia mazingira ya kifo chake lakini hayakuonesha kuvunjwa nyumba mahali popote.

“Polisi waliangalia umbali wa nyumba na choo ambako mke wa marahemu alikokwenda kujisaidia, na baada ya hapo walimchukua mke wa marahemu na watoto wanne ambao mpaka sasa wanashikiliwa” amesema mwenyekiti huyo.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Urlich Matei amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo yaliyohusishwa na familia ya marehemu.

Mtei amesema uchunguzi umebaini chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa eneo ambalo familia ilitaka kuuza na Mazinge alikuwa akikataa.

Wanaoshikiliwa na polisi ni mke wa marehemu, Chiku Mohamed (58), watoto wa marehemu, Salama Ally (20), Jumanne Ally (28), Idd Ally na Hawa Ally (22).

Mingange: Tupo tayari kuwakabili Sahare All Stars
Tanzania kupokea watalii kutoka China, India na Umoja wa Ulaya