Mahakama nchini Morocco imemhukumu kifungo cha miaka 12 jela, mwandishi wa habari maarufu, Taoufik Bouachrine baada ya kumtia hatiani kwa makosa ya unyanyasaji wa kingono na biashara haramu ya binadamu.

Bouachrine, ambaye ni mkurugenzi wa gazeti maarufu la Akhavar al-Yaoum, pia alihukumiwa kulipa faini ya 200,000 dirhams (sawa na $20,000). Hukumu dhidi ya mwandishi huyo ilitolewa Ijumaa ya wiki hii na Mahakama ya Rufaa jijini Casablanca.

Taoufik Bouachrine

Mwanahabari huyo mwenye umri wa miaka 49 alikamatwa Februari mwaka huu na polisi wa Casablanca ambao walivamia nyumbani kwake jijini humo.

Mwendesha mashtaka wa Serikali alisema kuwa kukamatwa kwa Bouachrine kulitokana na mfululizo wa malalamiko ya wafanyakazi wa kike wa kampuni yake ambao walikuwa wakimtuhumu kwa kuwanyanyasa kingono na kuwabaka.

Polisi walisema kuwa walikamata santuli 50 za ngono ambazo miongoni mwazo zinamuonesha Bouachrine akifanya mapenzi ofisini kwake. Tuhuma ambazo alizikanusha mara kadhaa.

Bouachrine alieleza kuwa mwanaume anayeonekana kwenye video hiyo sio yeye na kwamba waliopigwa picha za video kwenye mikanda hiyo wanaonekana wakiwa wanafanya mapenzi kwa makubaliano na sio ubakaji.

Kesi hiyo imekuwa ikikosolewa na wanaharakati ndani ya nchi hiyo wanaodai kuwa inamashinikizo ya kisiasa.

Wanawake wanne ambao walikuwa wametajwa kuwa walimlalamikia Bouachrine walijitokeza hadharani na kukana madai hayo.

Mwanamke mmoja alihukumiwa kifungo cha miezi sita jela kwa madai kuwa amepinga taarifa halali nay a kweli ya polisi kuhusu yeye kumlalamikia Bouachrine kuwa alimbaka.

Picha: Polisi waonesha nyumba aliyofichwa Mo Dewji alipotekwa
NECTA yatangaza tarehe ya kuanza mitihani kidato cha pili