Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga, Edward Bukombe amethibitisha kutokea kwa tukio la mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Old Tanga, Shufaa Mbughuni kuuawa kwa kuchunwa ngozi katika mtaa wa Majani Mapana Kata ya Nguvumali saa 9.40 alasiri.

Baba wa mwanafunzi huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Majani Mapana, Salim Mbughuni alisema bintiye aliwaaga wenzake juzi saa mbili usiku kwamba anakwenda kujisomea lakini hakurudi kama ilivyo kawaida yake.

“Aliwaaga wenzake kwamba anakwenda kujisomea na atarudi baada ya muda mfupi lakini hakuweza kurejea hadi mwili wake ulipoonekana siku ya pili mtaani hapa akiwa amefariki dunia,” alisema Mbughuni.

Mmoja wa wanafunzi katika shule hiyo, Halima Juma alisema: “Mimi usiku ule nilipigiwa simu ya kuulizwa kama nilimwita Shufaa lakini ukweli ni kwamba sikumwita. Leo hii rafiki yangu ameuawa kikatili namna hii inasikitisha sana.”

Aidha, Kamanda Bukombe amesema taarifa kamili kuhusiana na tukio hilo itatolewa mara baada ya madaktari wa Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo kuuchunguza kwa kina mwili huo.

“Ni kifo chenye utata hatuwezi kusema ameuawa au vinginevyo, tunasubiri taarifa ya madaktari wa Hospitali ya Bombo watakapouchunguza mwili huo; nitawaeleza habari yote,” amesema Bukombe.

Misri yapitisha sheria mpya ya mtandaoni, tovuti 500 zafungiwa
Diva aomba kuchangiwa Dola 7000 kujitibu, 'Nimelia sana'