Mwalimu Peter Makya Tabichi, anayefundisha katika shule ya Sekondari ya Kutwa ya Kericho iliyoko Nakuru nchini Kenya, ameshinda tuzo ya ‘Global Teacher Prize 2019’ iliyotolewa Jana jioni, Machi 24 nchini Dubai.

Mwalimu huyo ambaye hufundisha masomo ya hisabati na fizikia kwenye shule hiyo iliyoko katika kijiji cha Pwani, alipewa kiasi cha $1 milioni (Sawa na Shilingi bilioni 2.35 za kitanzania) kwa kutambua mchango wake katika jamii.

Taasisi ya The Varkey Foundation ilimtunuku mwalimu Tabichi tuzo hiyo kutokana na kufanya kazi kwa namna ya kipekee kusaidia jamii inayomzunguka pamoja na wanafunzi wake, tuzo hiyo hushindaniwa na washiriki kutoka duniani kote.

Mwalimu Tabichi mwenye umri wa miaka 36, amekuwa akitoa asilimia 80 ya mshahara wake wa ualimu kwa ajili ya kusaidia miradi ya kijamii ikiwa ni pamoja na elimu, kilimo na kuhuisha amani na utulivu.

“Amebadili maisha ya wanafunzi wake kwa namna nyingi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha klabu za sayansi na kuhimiza amani kati ya makundi mbalimbali ya kikabila na dini. Amesaidia pia kupambana na tatizo la baa la njaa katika jamii yake hususan eneo la Rift Valley,” taasisi hiyo ya Varkey Foundation ilisema wakati wa kumtangaza kuwa mshindi.

“Jitihada zake zimeisaidia shule yake ambayo iko maeneo ya vijijini kuzishinda shule bora zaidi nchini humo katika mashindano ya masomo ya sayansi, ameinua vipaji vingi vya wanafunzi wake na kuwafanya kuwa bora zaidi,” iliongeza.

Muigizaji maarufu  Hugh Jackman ndiye aliyemtangaza mwalimu Tabichi kuwa mshindi kwenye tukio hilo lililoitwa Global Education and Skills Forum.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alimpongeza mwalimu Tabichi kwa ushindi huo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari.

“Kwa niaba ya Wakenya, nichukue fursa hii kukukupongeza kwa kushinda tuzo ya Global Teacher wa mwaka 2019. Wewe ni mfano unaong’aa wa namna ambavyo unaweza kufanikisha sio tu kwa Kenya, sio tu kwa Afrika bali kwa dunia,” alisema Rais Kenyatta.

“Peter ulichagua kufundisha vijijini na ukayabadili maisha ya watu katika sehemu kama hiyo. Uamuzi ambao naamini ulikuwa mgumu. Unanipa matumaini kwamba wakati bora zaidi kwa Afrika uko mbele yetu na simulizi lako litawasha mwanga kwa vizazi vijavyo,” aliongeza.

Ajinyonga muda mfupi baada ya kuandika ujumbe Facebook
Live: Rais Magufuli akutana na Taifa Stars Ikulu baada ya ushindi 3 - 0 dhidi ya Uganda

Comments

comments