Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji unaolenga kuinua tasnia ya sanaa nchini ili kuendana na ushindani wa soko la kimataifa na kutoa ajira zaidi.

Dkt. Mwakyembe aliyasema hayo Ijumaa kupitia hotuba yake iliyosomwa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fissoo aliyemuwakilisha katika uzinduzi wa kampuni ya filamu na muziki ya Starline Films iliyoko Mikocheni B jijini Dar es Salaam.

Kupitia hotuba hiyo, aliipongeza menejimenti ya Starline Films ambayo inaongozwa na vijana wa Kitanzania kwa kazi nzuri za awali ambazo wamezifanya, kwani aliwahi kuitembelea miezi minne iliyopita na kuoneshwa baadhi ya kazi na uwekezaji unaokidhi matakwa ya soko la kisasa.

“Nimeambiwa asilimia 90 ya watendaji wa Starline Films ni vijana. Nimefurahi na nimefarijika kwa namna ambavyo vijana hawa wa Kitanzania walivyoweza kujitolea na kuendesha kampuni hii ya kisasa inayojihusisha na utayarishaji wa filamu, muziki pamoja na matangazo. Ni dhahiri, hatua hii imetokana na mazingira rafiki ya uwekezaji hususan kwa Watanzania, ambayo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kuiboresha sekta ya sanaa nchini,” alisema Dkt Mwakyembe.

“Kwa niaba ya Serikali, na kuzingatia Sera ya Tanzania ya Viwanda, napenda kueleza kuwa tunaitambua kampuni hii kama kiwanda kinachochakata na kuzalisha kazi za sanaa ya muziki na filamu pamoja na matangazo. Hivyo, ni hatua nzuri ya kuunga mkono jitihada na dhamira ya Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Niwahakikishie kuwa Serikali inawaunga mkono kwa hatua hii na itawasaidia kwa kadiri iwezavyo katika kuhakikisha wanapiga hatua mbele, na kuwa hamasa kwa makampuni mengine kuiga mfano huu,” aliongeza.

Alitoa rai kwa makampuni nchini kuwaamini vijana wa Kitanzania waliowekeza katika ubora wa kazi na ubunifu, kuwapa kazi ili kuwaunga mkono na kuchangia maendeleo ya tasnia ya sanaa nchini ambayo inatoa mchango mkubwa wa ajira unaochangia katika juhudi za kulisogeza Taifa katika uchumi wa kati.

Aidha, Dkt. Mwakyembe aliwataka wasanii kuhakikisha wanazingatia Sheria na maadili ya Kitanzania kwa kutayarisha filamu zenye jumbe zinazojenga jamii bora na sio kubomoa jamii. Alisisitiza kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua wasanii ambao wataenda kinyume na matakwa ya sheria, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha kazi zao Bodi ya Filamu kwa ajili ya ukaguzi kabla ya kuingia sokoni, pamoja na kuwasilisha kazi za muziki BASATA.

Pia, aliwahakikishia wadau wa sanaa ya filamu na muziki kuwa Serikali kupitia vyombo vyake itaendelea kupambana na wizi wa kazi za wasanii pamoja na aina zote za unyonyaji. Alisema kuwa ili kupata uhalali na ulinzi dhidi ya kazi zao na jasho lao, wasanii wote wanapaswa kuzingatia matakwa ya sheria kwa kusajiliwa na Bodi ya Filamu kwa waigizaji, na wasanii wote kwa ujumla kusajiliwa na kutambuliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fisso (aliyekaa-kulia), pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Starline Films, Silver Oddo katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa kampuni hiyo

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Staline Films, Silver Oddo aliishukuru Serikali kwa kazi nzuri inayofanyika katika kurasimisha tasnia ya sanaa nchini pamoja na kusaidia kuhuisha mazingira bora ya uwekezaji, ulezi na usimamizi wa kazi za sanaa.

Oddo aliyaalika makampuni ya umma na binafsi pamoja na wadau wa sanaa kwa ujumla, kuiamini kampuni hiyo kwani wanatumia teknolojia ya kisasa, vifaa bora na vipaji kuzalisha kazi zenye kiwango cha ushindani wa soko la kimataifa.

“Kama Mgeni Rasmi na wadau wote mlivyojionea hapa, kazi zetu ni za ubora unaokidhi mahitaji ya soko la kisasa. Ukifanya kazi nasi iwe ya matangazo, filamu, makala au muziki hakika utaona thamani ya fedha yako,” alisema Oddo.

Aliongeza kuwa wanatarajia kuanza kurusha kipindi kinachoitwa Mr. Director hivi karibuni kupitia East Africa TV (Channel 5), kitakachoonesha ubora na utofauti mkubwa wa utayarishaji wa kazi za sanaa unaokidhi soko la kisasa na kuhimili ushindani wa kimataifa. Hivyo, aliyaalika makampuni kuwekeza kwa kudhamini kipindi hicho.

Takribani watu maarufu 90 walihudhuria uzinduzi huo, wengi wakiwa wasanii maarufu kama Mzee Chillo, Natasha, Chausiku, Dude, JK Comedian, Rose Ndauka, Mzee Almas na wengine. Pia, wawakilishi wa makampuni mbalimbali ya umma na binafsi walihudhuria, ikiwemo TTCL walioahidi kuendelea kushirikiana na makampuni na wasanii wa Tanzania kupeleka jumbe zao kwa wateja.

Muangalie Mama Fisso katika moja ya mahojiano aliyofanya na Dar24 usiku huo:

Tyson Vs Wilder laishangaza dunia, washindwa kupata mbabe
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Desemba 2, 2018

Comments

comments