Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amesema kuwa Mvua zinazoendelea kunyesha wilayani Kyela zimesababisha uharibifu wa makazi ya watu na majengo hasa shule ya msingi na sekondari ya Mwaya zilizopo katika kata ya Mwaya ambazo zote mpaka sasa zimezingirwa na maji.

Amesema kuwa katika wilaya ya Rungwe maeneo ya Igamba, Tukuyu mjini imesababisha maafa ikiwemo kubomoka kwa nyumba za wakazi wa maeneo hayo.

Mvua hizo zinazoendelea kunyesha katika Wilaya za Rungwe na Kyela zimesababisha Maafa ikiwemo nyumba kuezuliwa, mifugo kusombwa na Maji pamoja na uharibifu wa mazao ukiwemo mpunga na kusababisha baadhi ya shughuli za Maendeleo kusimama.

Wakizungumza na Dar24 Media, wananchi wanaoishi katika Kata za Mwaya,Tenende na Ipande wilayani Kyela wamesema kuendelea kunyesha kwa Mvua hizo kunaweza kusabababisha hatari kubwa zaidi kwani mpaka sasa baadhi ya nyumba zimeezuliwa na mifugo imesombwa na maji.

Wamesema kuwa Mvua hizo zimesababisha kukatika kwa mawasiliano kwenye barabara Ipinda- Matema katika eneo la Tenende ambayo ilizinduliwa hivi Karibuni na Rais Dkt. John Magufuli.

Aidha eneo la Tenende ambalo ndio tegemeo kwa kilimo cha Mpunga kwa kiasi kikubwa limeathiriwa na mvua na kusababisha Mpunga kufunikwa na maji hali inayoleta wasiwasi kwa wakulima.

“Tunashindwa kusafiri kwenda Kyela mjini Kwasasa kwasababu ya kukatika kwa mawasiliano ya barabara katika kipande cha Tenende hivyo inatulazima kutumia kuvuka upande wa pili, tunaomba eneno hili lifanyiwe marekebisho ili kuondoa kero hizi,”wamesema wananchi hao.

Hata hivyo, kamanda Matei amewataka wazazi na walezi na wananchi kwa ujumla kwa makini kupita maeneo yenye mafuriko na kuhakikisha watoto hawachezi katika maeneo hatarishi ikiwemo ya mito au mabwawa.

Vitambulisho vya JPM kutumika kwenye mikopo Njombe
LIVE: Yanayojiri Bungeni jijini Dodoma leo Mei 15, 2019