Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema ushindi wa Donald Trump kuwa Rais wa Marekani kupitia uchaguzi uliopita umetokana na laana ya Afrika na Mashariki ya Kati kwa taifa hilo.

Kupitia tamko lake lililosambaa kwenye vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na BBC, Rais Museveni amesema kuwa kwa kipindi kirefu Marekani, Uingereza na nchi marafiki zao wamekuwa wakikandamiza mataifa ya Afrika na Mashariki ya Kati, hivyo wamepata pigo la laana ya kisiasa.

“Ingawa kuna sababu nyingine ambazo sisi watu wa nje hatuwezi kuzifahamu kirahisi, kuna sababu moja ambayo imebadilika kuwa laana kwa mataifa haya makubwa [Marekani na Uingereza],” ameandika.

Amesema Marekani imepata laana ya kisiasa kutoka kwa mataifa ambayo ilianzisha vita isiyo na msingi dhidi yake. Alizitaja vita ziliyoratibiwa na Marekani dhidi ya Iraq na Libya kuwa hazikuwa za haki.

Aliongeza kuwa laana ya vita hizo ndizo zilizopelekea pia aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza kupata janga la kujiuzulu baada ya wananchi wake kuamua kujiondoa katika Umoja wa Ulaya kupitia kura ya maoni, huku Marekani, Hillary Clinton akishindwa uchaguzi.

“Iwe iwavyo, waliochagiza mashambulizi mashariki ya kati na kaskazini mwa Afrika, waliibua majanga na laana ambazo zilipelekea kuangushwa kwa Clinton na Cameron,” linaeleza tamko la Museveni.

Museveni ni mmoja kati ya marais wa Afrika ambao walimpongeza Trump kwa kushinda uchaguzi wa Urais na kuwa Rais Mteule wa taifa hilo lenye nguvu zaidi duniani.

Casimiro Aongeza Nguvu Real Madrid
#HapoKale