Diamond Platinumz ameitoa kimasomaso Afrika Mashariki kwenye tuzo za MTV/MAMA2015 zilizofanyika jana, Julai 18, Durban, Afrika Kusini ambapo alinyakua tuzo ya Best Live Act.

Diamond alishinda tuzo hiyo ikiwa ni kati ya tuzo tatu alizotajwa kuwania. Best Male Artist iliyoenda kwa Davido, na Best Collaboration iliyoenda kwa AKA feat. Burna Boy (All Eyes On Me).

Kwa kuwa ndiye mshindi pekee wa tuzo hizo kutoka Afrika Mashariki kwa mwaka huu, mtoto wa Tandale amepata pongezi kutoka pande zote za Afrika na sehemu nyingine za Dunia kwa ujumla.

Lakini kwa upande wa Tanzania imekuwa tofauti kidogo. Pongezi hizo zimeibua zaidi joto la mashambulizi na mgawanyiko kati ya zile team za mitandaoni, yaani Team Diamond na Team Ali Kiba ikiwa ni siku chache baada ya wasanii hao kusistiza zaidi ya mara moja kuwa hawana bifu.

Ukweli wa kuwepo joto la uhasama aka bifu kati ya timu hizo mbili unaanza kuonekana kuanzia kwenye post zinazowekwa na watu wa karibu wa Diamond ama Diamond mwenyewe ambazo kwa mtazamo wa kawaida ni dhahiri kuwa zinarusha makombora upande wa pili.

Post iliyowachanganya wengi ni ile ya Babu Tale inayomuonesha Diamond akiwa amepozi na mameneja wake, Babu Tale, Salaam na Said Fella ambapo Diamond anaonekana akiwa ameonesha ‘dole la kati’, kitu kinachoeleweka wazi kuwa ni tusi kubwa.

“Unaweza kudanganya watu kwa muda mfupi..lakini huwezi kudanganya watu kwa muda wote..Asante MTV kwa kutambua juhudi zetu,” aliandika Babu Tale kwenye post hiyo.

Matusi makali yaliporomoshwa yakifuatana na pongezi kutoka kwa wale die hard fans ambao kwao kidole hicho sio ‘focal point’. Lakini pia wapo walioandika ushauri kwa lugha nzuri bila matusi katika post hiyo.

Diamond pia alipost kijembe kingine kwenye akaunti yake akiwaacha mashabiki kuamua cha kuandika.

“Mbona Bado Mtanyooka tu…” ameandika Diamond kwenye post yenye video inayomuonesha Jokate Mwegelo akicheza na kusherehekea na wimbo wake ‘Mdogomdogo’. Japo hii ni baada ya kupost akiwashukuru mashabiki wake, vyombo vya habari na wasanii wenzake wote (ina maana wote bila timu).

Post hiyo inayomuonesha Jokate ambaye wengi wanaamini ni timu Kiba japo aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Diamond iliwachanganya mashabiki wengi walioonekana kutofautiana kimtazamo, ni video ya zamani au party ya jana?

Mbona Bado, Mtanyooka tu…

A video posted by Chibu Dangote.. (@diamondplatnumz) on

Bila shaka hiyo ni video ya zamani ambayo Diamond ameitumia kuimaliza nguvu kambi ya wapinzani wake ambao hivi karibuni alisema hana bifu nao, lakini vitendo vimeonesha wazi kuwa hii ni vita ya timu inayopoozwa kupisha mambo fulani yapite ianze tena.

Comments zinazoporomoka chini ya post hiyo zimejaa ushabiki wa timu na matusi yasiyo na maana kutaka kukomoana huku majina ya watu maarufu waliowahi kuonekana kuwa mstari wa mbele kusapoti pande za timu hizi yakitajwa mara kwa mara.

Hali hiyo pia imeibuka kwenye post ya Ali Kiba ambaye hata hivyo hakumpongeza Diamond Platinumz kwa ushindi wake kama wafanyavyo wasanii wengine wengi, ingawa kumpongeza ama kutompongeza sio sheria.

Ni kama vile mashabiki walikuwa wanatafuta sehemu ya kuandika kwenye eneo la Ali Kiba na mwisho kuivaa post yake akiwa na familia yake ndani ya mavazi rasmi kuadhimisha sikukuu ya Eid. Zilifuata comments zaidi ya 687 ambazo asilimia 97 zilikuwa zinabishana na kuchanana kuhusu ushindi wa Diamond Platinumz kwa mtazamo wa ushabiki wa timu zao.

Comments kama hizo zimeendelea pia kwenye post ya Wema Sepetu ambaye katika lile vuguvugu alionekana kuwa upande pinzani wa Diamond huku harakati zake kwenye mtandao zikitajwa kuwa moja kati ya kampeni zilizomuwezesha Ali Kiba kushinda tuzo nyingi zaidi za KTMA2015.

Tukiachana na joto la timu, Diamond amepiga hatua kubwa zaidi kwenye maisha yake ya muziki na sasa tunatarajia kupata collabo za nje ya Afrika huku tukiwa na matumaini ya collabo ya kwanza kati yake na mkali wa ‘Miss Independent’, Ne-Yo. Nyingi zitakuja.

My Take: Ni dhahiri kwamba Diamond na Ali Kiba bado hawajamalizana, sio tu kwamba timu zao ndizo huchochea bifu lao kama wengi tulivyokuwa tunafikiria na kuyanunua maneno matamu waliyokuwa wakiyaongea kwenye media hivi karibuni. “Sina na sijawahi kuwa na bifu nae,” Diamond aliiambia XXL ya Clouds Fm. Ali Kiba nae vilevile huku wakirusha lawama kwa timu zao kwenye mitandao ya kijamii.

Kama kweli hamna bifu… Ali Kiba angefanya kitu kumpongeza msanii mwenzake kwa tuzo nzito aliyoibeba, kiroho safi. Hapo timu zote zingenyamaza kwa sababu vitendo vinaonesha kweli hamna bifu. Kama alivyofanya Davido kwa Diamond na Wizkid.

Kwa macho ya wazi (naked eyes) na akili ndogo tu ya kuiangalia hii, unaweza kuona kuwa Diamond amemuatack Ali Kiba moja kwa moja na watu wake kwa post hizo, hasa baada ya kutumia video ya zamani ya Jokate na kuonesha dole ambalo sio utamaduni wa Afrika. Unamtukana nani kaka? Sisi mashabiki tuliovote au mahasimu wako ambao tunajua moja kwa moja ni timu Ali?

Diamond anao uhuru wa kuandika na kupost chochote kwenye page yake, lakini akumbuke kuwa yeye ni mtu mwenye ushawishi mkubwa sana kwenye jamii yetu hivi sasa. Hivyo, kila awekacho kwenye mitandao yake kwa ajili ya umma huacha madhara hasi au chanya kwa wengi.

Mwisho, nakupongeza sana Diamond Platinumz kwa kutuwakilisha vyema, tunasubiri kubeba tuzo nyingine kubwa zilizo mbele yako. Tayari umeshatajwa kuwania tuzo kubwa za Nigeria Entertainment Awards za Marekani na tuzo nyingine zitakazotolewa Uganda. Bidii ya kazi, ubunifu, kipaji na sapoti ya watanzania ndio siri kubwa ya kukufikisha hapo.

‘Safari Ya Matumaini Yahamia Ukawa’
Ray C Aweka Wazi Hisia Zake Kwa Rais Kenyatta, ‘Huwa Namuota ’