Michel Gbagbo, mtoto wa rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela na faini ya $950 baada ya kukutwa na hatia ya kusambaza habari za uongo.

Katika kesi ya msingi, Michel alidaiwa kutoa habari za uongo kupitia mahojiano aliyoyafanya mwaka 2016 kupitia tovuti moja maarufu, ambapo alidai kuwa watu 250 wanashikiliwa magerezani kufuatia vuguvugu la mwaka 2010-11 wakati baba yake alipokataa kutoka madarakani baada ya kushindwa na mpinzani wake, Alassane Ouattara.

Mtoto huyo pia alieleza kwenye mahojiano hayo kuwa zaidi ya watu 300 waliokamatwa wakati huo na kufunguliwa mashitaka tangu mwaka 2011 wamepotea.

Hata hivyo, leo mahakama ya makosa ya jinai nchini humo imeamuru kuwa maelezo yote yaliyotolewa na Michel yalikuwa ya uongo kutokana na ushahidi uliowasilishwa hivyo ikampa adhabu.

Rungu la sheria pia lilimuangukia mkurugenzi wa tovuti hiyo ya ‘koaci’ inayorusha habari kwa lugha ya kifaransa, ambapo amepigwa faini ya $18,950 kwa kusambaza habari za uongo.

Wanasheria wa Michel wameeleza kuwa watakata rufaa dhidi ya maamuzi hayo ya mahakama.

Chuo Kikuu Zimbabwe chaanika ‘Research ya PhD’ ya mke wa Mugabe
Moto wateketeza wagonjwa hospitalini