Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amemteua Julius Mtatiro kuwa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tunduru iliyoko Mkoani Ruvuma.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, uteuzi wa Mtatiro unaanza rasmi leo, Julai 14, 2019.

Amechukua nafasi ya aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo, Juma Homera ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi.

Mtatiro aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama Cha Wananchi (CUF), akiwa kwenye kambi iliyokuwa inamuunga mkono aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad wakati chama hicho kilipokuwa kwenye mgogoro wa uongozi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa.

Mwaka 2015, aligombea ubunge wa Segerea kupitia chama hicho alichokitumikia kwa kipindi cha takribani miaka 10. Aliungwa mkono na vyama vya upinzani vilivyounda Ukawa, lakini kura alizozipata hazikutosha kumpa ushindi.

Agosti 2018, alitangaza rasmi kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) akieleza kuwa uamuzi wake unatokana na kuridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Rais Magufuli.

Mtatiro ambaye kitaaluma ni mwanasheria, ni miongoni mwa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa na uwezo wake wa kuchambua na kuwasilisha mada mbalimbali umempa heshima kwenye ulingo wa siasa.

Mbali na kusimama kwenye majukwaa, Mtatiro alikuwa akiandika mawazo yake kwenye gazeti la Mwananchi akichambua kinagaubaga mambo mbalimbali yanayoligusa taifa kwa ujumla. Kadhalika, ukurasa wake wa Facebook ulikuwa uwanja wenye ushawishi kwa watu wengi kuhusu masuala ya kisiasa, uchumi na mambo mengine ya kijamii.

Hata hivyo, Mtatiro sio wa kwanza aliyetoka katika kambi ya upinzani, kuhamia CCM na kupewa ‘shavu’ kubwa.

Baadhi ya waliopata nafasi ya kuteuliwa, waliohama kutoka upinzani na kujiunga na chama tawala ni pamoja na Mwita Waitara (Naibu Waziri Tamisemina Mbunge wa Ukonga), Patrobas Katambi (DC-Dodoma Mjini) aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana-Chadema, David Kafulila (Katibu Tawala-Songwe) aliwahi kuwa Mbunge machachari wa NCCR-Mageuzi.

Orodha ni ndefu lakini wote ni wanasiasa wenye uwezo mkubwa ambao mchango wao umewahi kuonekana hata walipokuwa wakitumikia vyama hivyo vya upinzani, na sasa wako ndani ya Serikali wakitoa mchango wao.

Tunamtakia kila la kheri kwenye uteuzi wake mpya.

Prof. Mbarawa awasukuma ndani waliotafuna pesa za mradi wa maji
Julius Mtatiro ateuliwa kuwa DC wa Tunduru

Comments

comments