Mbunge wa Geita vijijini, Joseph Kasheku maarufu kama Msukuma amewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliopewa dhamana ya kukisemea chama hicho, kuiga mfano wa aliyekuwa Katibu Mwenezi CCM, Nape Nnauye kupambana na hoja za wapinzani.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Msukuma ambaye ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita amesema kuwa hoja zilizotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu akidai ndege ya Tanzania aina ya Bombardier Q400 imeshikiliwa nchini Canada ni za uongo na za kisiasa, hivyo zilipaswa kujibiwa na wanasiasa wa CCM.

Alisema kuwa viongozi hao wanapaswa kuisadia Serikali ya Rais John Magufuli kujibu hoja za kisiasa za wapinzani zenye lengo la kuvuruga mipango ya maendeleo.

“Na mimi niwaombe wana CCM wenzangu mliopewa nafasi ya kutusaidia kuzungumza, suala linapokuja la kisiasa msimuache Mheshimiwa Rais akahangaika na Serikali yake. Tusimame kama wanasiasa tujibu. Mtu wa Serikali hawezi kujibu kisiasa kama alivyojibu Tundu Lissu,” alisema.

“Wasimame watu waliopewa nafasi hizi kwenye chama. Wapo Wenezi wa kitaifa na watu wanaoweza kusimama kupambana kujibu hizi hoja. Kwanini hatujifunzi kwenye kipindi kilichopita, yalikuwa yakizungumzwa haya Nape anajibu kesho yake,” aliongeza.

Msukuma alisema kuwa wanasiasa wa upinzani wameleta hoja hii kuleta mtikisiko ili wadai wa Serikali waliowasilisha pingamizi Mahama za Kimataifa waweze kulipwa fedha na kuwapa asilimia kumi (10%).

Alisema kuwa anaamini Serikali ya Rais Magufuli itafanya mazungumzo na walalamikaji waliowasilisha ombi la zuio la ndege hizo na kuwalipa kiasi cha fedha na suala hilo litamalizika.

Video: Rais Shein alivyowafunda wanafunzi kuhusu yanayowazidi umri
Pep Guardiola Kupambana Na Hali Yake