Mahakama ya Tanzania imependekeza makosa yote kuwa na dhamana kwa kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa msongamano wa Mahabusu kwenye Magereza mbalimbali nchini.

Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kuwaapisha wanasheria waliomaliza mafunzo ya Sheria kwa vitendo kuwa Mawakili, ambapo amesema kuwa baadhi ya mapendekezo ya Mahakama yatakayosaidia kuondoa msongamano magerezani kuwa ni pamoja na upelelezi wa kesi kumalizika mapema.

Amesema kuwa Mahakama imekuwa ikilaumiwa kwa kuchelewesha kesi mahakamani lakini kinachosababisha kuchelewa kwa mashauri hayo ni upelelezi kutokukamilika kwa wakati.

“Kuchelewa kumalizika kwa shauri Mahakamani wa kulaumiwa ni wapelelezi na siyo Mahakama,” amesema Jaji Mkuu Prof. Juma.

Amesema kuwa pendekezo jingine ni sheria kutamka wazi muda wa kufanya upelelezi yaani ikifika muda fulani upelelezi haujakamilika basi shauri hilo lifutwe mahakamani.

Aidha, ameongeza kuwa sheria zimeegemea zaidi kwenye adhabu kubwa huku akitolea mfano wa mashauri ya mauaji, matumizi ya dawa za kulevya, Uhujumu uchumi na ubakaji, ambapo amesema kuwa mashauri hayo yana adhabu kubwa na upelelezi wake huchukua muda mrefu.

Pia amesema ili kutatua changamoto ya msongamano wa mahabusu magerezani, Mahakama ya Tanzania inapendekeza masharti ya dhamana kulegezwa na kushauri kutumiwa kwa vitambulisho vya Taifa kwenye dhamana.

“Hivi sasa wananchi wengi wana vitambulisho vya Taifa ambavyo vinaweza kutumika kama dhamana bila ya kumtaka mwananchi aonyeshe mali,”ameongeza Prof. Juma.

Hivi karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli aliagiza kufanyika kwa uhakiki ili kubaini mahabusu na wafungwa waliobambikiwa kesi hatimaye kuachiwa huru. Watakaonufaika na matokeo ya uhakiki huo ni mahabusu wenye kesi ndogondogo na wafungwa watoto, wazee, na makundi mengine yenye mahitaji maalum.

Jumla ya wanasheria 720 wamekubaliwa na kuapishwa kuwa Mawakili wakiwemo Majaji nane wa Mahakama ya Rufani, Majaji saba wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Majaji wastaafu watatu, Manaibu Wasajili kadhaa, Mahakimu pamoja na wanasheria wengine.

Hii ni mara ya 60 kwa Mahakama ya Tanzania kuwakubali na kuwaapisha Mawakili wapya. Kwa mara ya kwanza Mahakama ya Tanzania iliwakubali na kuwaapisha Mawakili wapya mwaka 1986.

LIVE KILIMANJARO: Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika Uzinduzi wa Treni ya Mizigo kutoka DAR ES SALAAM- TANGA-KILIMANJARO
Waziri mkuu amsimamisha mhandisi wa maji