Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara msimu wa 2016/2017 inatarajiwa kuendelea kesho Jumamosi Septemba 17, 2016 kwa michezo sita ambayo itazikutanisha timu pinzani 12 katika viwanja sita tofauti.

Michezo ya kesho ni Mwadui FC itakayoikaribisha Young Africans kwenye Uwanja wa CCM Kambarage. Mwadui ambayo inaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Stand United wakati Young Africans ina makali ya kuilaza Majimaji ya Songea mabao 3-0.

Mechi nyingine yenye mvuto ni kati ya Tanzania Prisons kuwa mgeni wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya wakati Azam ambayo inaongoza ligi sawa Simba kwa kuwa zina pointi sawa, zitakutana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Timu za Simba na Azam zina pointi 10 kila moja baada ya kucheza mechi nne ambako kila moja imeshinda mechi tatu na kutoka sare mmoja.

Mtibwa Sugar na Kagera Sugar zinatarajiwa kukutana kwenye Uwanja wa Manungu kwenye mchezo mwingine wa Ligi Kuu. Mtibwa ambayo imetoka kulazwa na Simba Jumapili iliyopita, Kagera inakwenda ugenini Morogoro ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare tasa na Ndanda ambayo pia kesho itakuwa ugenini kucheza na Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Majimaji.

Katika mchezo mwingine wa kesho, Ruvu Shgooting itakuwa mwenyeji wa Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani wakati Keshokutwa Stand United ya Shinyanga itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa CCM Kambarage.

Mzunguko wa tano wa ligi hiyo utafungwa kwa mchezo kati ya African Lyon ya Dar es Salaam dhidi ya Toto African ya Mwanza kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam Jumanne Septemba 20, 2016. African Lyon inaingian uwanjani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuilaza Mbao FC mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Malinzi Ampongeza Rais Mpya UEFA
Waziri Mkuu apokea sh. mil. 121.679 kusaidia waathirika tetemeko la ardhi Kagera