Msajili na Mkurugenzi wa Idara ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Vickness Mayao amewatoa hofu wadau wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali nchini kuwa Serikali haina nia mbaya na Mashirika hayo ila inataka iwe na utaratibu mzuri wa kuyaratibu Mashirika hayo.

Ameyasema hayo jijini Dar Es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na zoezi la usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali linaloendelea jijini Dar es Salaam kwa Kanda ya Mashariki.

Amesema kuwa utaratibu wa usajili umerahisishwa sana hasa ule wa Mashirika yaliyokuwa yamesajiliwa katika Sheria nyingine.

Ameongeza kuwa Wadau wameridhishwa na huduma zinazotolewa na Ofisi yake na kusema wanapata mrejesho mzuri kutoka kwa wadau kupitia fomu za mrejesho wa zoezi hilo.

Kwa upande wake mdau kutoka Taasisi ya Solidame Ifakara, Ali Mzava ametoa rai kwa wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaliyosajiliwa chini ya Sheria nyingine kujitokeza kwa wingi kujisajili chini ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwani usajili umeboreshwa na hakuna tatizo lolote katika zoezi hilo.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Tanzania Community Development Assistant, Denis Mchunguzi amesema kuwa wadau wameyapokea vizuri mabadiliko ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 3 ya Mwaka 2019 kwani wameitikia wito na kujitokeza kwa wingi na hawana tatizo na utekelezaji wa marekebisho ya Sheria hiyo.

Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali inaendelea na zoezi la usajili wa Mashirika yaliyosajiliwa awali chini ya Sheria nyingine kama vile “Societies Act Cap 337” (Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi); “Trustees’ Incorporation Act Cap. 318 (RITA); na The Companies Act Cap 212 (Msajili wa Makampuni-BRELA) ambazo zinatakiwa kujisajili chini ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria Na. 3/2019.

Usajili huo umeanza katika Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Pwani na Morogoro) na Kituo kitakuwa Ofisi za Wizara ya Afya-Dar es Salaam kuanzia tarehe 10-19/07/ 2019.

LIVE MWANZA: Rais Magufuli katika uzinduzi wa huduma za tiba hospitali ya Rufaa Bugando
LIVE SENGEREMA: Rais Magufuli akizungumza na Wananchi

Comments

comments