Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesema kuwa wizara yake haina mpango wa kuongeza tena muda zoezi la utambuzi wa mifugo na kuwataka wafugaji popote walipo nchini kupaza sauti zao ili kuhakikisha kuwa ng’ombe na punda wote wamepigwa chapa ifikapo Januari 31 mwaka huu.
Ameyasema hayo hii leo mjini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa tathmini ya utekelezaji wa zoezi upigaji chapa mifugo mpaka kufikia Januari 16 mwaka huu jumla ya ng’ombe 10,306,359 sawa na asilimia 59.3 ya lengo wameshapigwa chapa ikiwa ni ongezeko la asilimia 20 ya tathmini ya awali.
Aidha, amesema wafugaji wote nchini wataoshindwa kupiga chapa mifugo yao ndani ya muda uliowekwa hatua kali zitachukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji Namba 12 ya mwaka 2010 ibara ya 4 kifungu cha 26 huku akizionya halmashauri ambazo zitashindwa kutekeleza kikamilifu.
Amesema kuwa hadi sasa halmashauri 100 zimepiga chapa zaidi ya asilimia 50, halmashauri 54 zimepiga kati ya asilimia 10 hadi 50, halmashauri 14 zimepiga chini ya asilimia 10 huku  halmashauri 9 zikiwa bado hazijaanza kabisa zoezi hilo.
Hata hivyo, Mpina amezitaja Halmashauri hizo ambazo hadi sasa hazijaanza kupiga chapa ni Tandahimba, Nanyumbu, Mafia, Newala, Halmashauri za miji ya Newala, Nanyamba, Masasi na Manispaa za Kigamboni na Ilemela Mwanza.

Zamaradi awajibu wanaodai ‘ana-stress za mapenzi’
Mailu ataka ripoti hospitali inayodhalilisha wanawake kingono