Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina leo Jumatano, Juni 20, 2018 ameliomba radhi Bunge kwa kitendo cha maofisa wa wizara yake kuingia kwenye mgahawa wa Bunge jijini Dodoma na kupima kwa rula samaki waliopikwa kwa ajili ya kitoweo kinyume na taratibu za bunge.

“Napenda kukiri kwamba watumishi katika kutekeleza kazi hiyo waliingia bila kibali, kupima chakula kilichopikwa na kwa taratibu hizo, wizara inaliomba radhi Bunge lako tukufu na wewe mwenyewe.” Mpina.

Naibu spika wa Bunge Tulia Ackson amemshukuru waziri kwa maelezo aliyoyatoa na kusema kuwa Bunge limesikitishwa sana na kitendo hiko kilichofanywa na maofisa hao.

”Waziri mkuu tunasikitishwa sana na kilichotokea, sisi si Bunge pekee duniani, sisi ni jumuiya ya kimataifa, wenzetu wakisikia kuna waziri na maofisa walichofanya ni dharau ya juu sana,” amesema Naibu Spika.

Hata hivyo Spika wa Bunge Job Ndugai naye ameongezea kuwa kitendo kilichofanywa na maofisa hao cha kupima samaki na kuita waandishi wa habari ni kama kinaashiria mpango fulani wa kuliweka Bunge pasipostahili“

”Wapimaji wa wizara wanapima samaki mikono haina hata gloves, mikono wazi, wanashikashika, si wao peke yao, wamealika na waandishi wa habari, yaani ni kama mpango fulani wa kuliweka Bunge kusipostahili, kwa kawaida naomba tukubaliane nami, ukiwa umekasirika sana unapaswa kusamehe,”. amesema  Ndugai.

Jana Maofisa wa wizara hiyo walikamata samaki aina ya sato wasiofikia kiwango cha kuvuliwa kiasi cha kilo mbili kati ya 100 waliokuwa wakiuzwa kinyume cha sheria katika mgahawa wa ofisi ya Bunge ambapo walikuwa wakipima urefu wa samaki kwa kutumia rula ya daftari.

Baada ya hapo, mmiliki wa mgahawa huo, Daniel Lamba, alipigwa faini ya Sh. 300,000 baada ya kukiri kosa la kukutwa na samaki hao wachanga.

John Mpepele ambaye ni Msemaji wa wizara hiyo alisema walipata taarifa za kuwepo samaki hao kutoka kwa Waziri wa Wizara hiyo, Luhaga Mpina aliyekuja kwenye mgahawa huo juzi asubuhi.

 

Marekani yajitoa UN yadai ni baraza la kinafiki
Video: Barnaba, Vanessa waachia nyimbo yao mpya ''Chausiku'' itazame hapa