Waendesha mashtaka wa Marekani wanamtuhumu Monica Witt aliyekuwa afisa wa kikosi cha anga cha jeshi la nchi hiyo kwa kuasi na kuwa mpelelezi wa jeshi la Iran akiwalenga aliokuwa akifanya nao kazi awali.

Kwa mujibu wa waendesha mashtaka hao, Monica alivigeuka vikosi vya Marekani mwaka 2013 akitumia maarifa ya kipelelezi ya kijeshi kuhujumu jeshi la nchi hiyo.

Shirika la Ujasusi la FBI limeeleza kuwa mwanamke huyo alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na hati ya usalama wa hali ya juu alipokuwa akifanya kazi na jeshi la Marekani kati ya mwaka 1999 na 2013.

Aidha, watu wannne ambao ni raia wa Iran wamekamatwa kwa tuhuma za kujaribu kuweka program ya kipelelezi kwenye kompyuta zinazomilikiwa na Monica.

Idara ya Hazina ya Marekani pia imeyafungia makampuni mawili ya Iran ambayo ni New Horizon Organization na Net Peygard Samavat kwa tuhuma za kuhusika kuwezesha kifedha mpango huo wa Iran.

“Hii ni siku mbaya kwa Marekani, ambapo raia mwenzetu ameisaliti nchi,” alisema Mwanasheria Mkuu Msaidizi, John Demers.

Monica anadaiwa kuvujisha siri za ndani za jeshi la Marekani kwa Iran yakiwemo majina ya wapelelezi na taarifa za ndani za oparesheni kadhaa.

Kupitia nyaraka za mashtaka, wapelelezi wameeleza kuwa mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 39 alipelekwa Mashariki ya Kati kwa ajili ya kufanya kazi maalum zilizobeba oparesheni za siri.

 

 

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Februari 14, 2019
Waandishi wa habari wapotea, wengine wauawa barani Ulaya