Moto mkubwa umewaka ghafla kwa nyakati tofauti na kuteketeza vyumba vinne katika nyumba ya mkazi mmoja wilayani Njombe aliyefahamika kwa jina la Fredrick Kitalula na kusababisha hasara kubwa.

Mmiliki huyo wa nyumba hiyo ambaye ni Katekista wa Kanisa Katholiki, amesema kuwa moto huo awali ulianza kuwaka katika chumba anacholala mtoto wake wa kiume na kufika katika vyumba vingine bila kujua ni nini chanzo cha moto huo wakati nyumba yake haina umeme.

“Kwa kweli hata sielewi moto huu ulianzaje mimi niliona tu umeanza katika nyumba ya kijana wangu mpaka katika vyumba vingine japo tulifanikiwa kuuzima lakini bahati mbaya umeunguza nguo zote za watoto wangu, vitanda viwili na fedha shilingi elfu 90 ambazo nilizitenga kwa ajili ya kulipia ada ya mtoto mwezi ujao” amesema kitalula.

Kwa upande wake mke wa Katekista huyo, Nicolina Mkungilwa amesema kuwa kitendo cha kuungua nyumba yake imekuwa ni ajabu kwake kwani anashindwa kuelewa moto huo umetokeaji.

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ringabena kilichopo katika Kijiji hicho, George Mhadisa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku serikali yake ikijipanga kuisaidia familia hiyo ambayo imekutwa na janga hilo.

Vitambulisho vya JPM kuwaneemesha Wajasiliamali Ludewa
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Desemba 28, 2018