Aliyekuwa rais wa zamani wa Misri, Mohamed Morsi amezikwa mara baada ya kufariki dunia hapo jana akiwa mahakamani siku ya Jumatatu.

Wakili wake ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kuwa kiongozi huyo wa zamani amezikwa mashariki mwa jiji la Cairo asubuhi ya leo Jumanne.

Morsi,aliyekuwa na miaka 67, alikuwa kizuizini tangu alipoondolewa madarakani mwaka 2013.

Makundi ya watetezi wa haki za binaadamu , ambayo yalikosoa mazingira ambayo Morsi aliwekwa, wametoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi kuhusu kifo chake.

Aidha, mtoto wake, Abdullah Mohamed Morsi, ameliambia shirika la habari la Uingereza, Reuters kuwa siku ya Jumatatu mamlaka za Misri ziliikatalia familia yake kufanya maziko katika mji yalipo makazi yake.

Kiongozi wa juu wa zamani wa kundi lililopigwa marufuku nchini humo, Muslim Brotherhood, Morsi alikua kiongozi wa kwanza kuchaguliwa katika kiti cha urais kwa njia ya Demokrasia mwaka 2012, lakini aliondolewa na kushikiliwa baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka mmoja baada ya kufanyika maandamano makubwa kupinga utawala wake.

Hata hivyo, Abdul Fattah al-Sisi, kiongozi wa zamani wa jeshi, ndiye rais wa sasa wa Misri ambapo amekuwa madarakani tangu mwaka 2014, baada ya kumpindua Morsi.

Muslim Brotherhood na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, mshirika wa karibu wa Morsi wameulaumu utawala wa Misri kuhusu kifo cha Mohamed Morsi.

Ujangili wapungua kwa 70%, Waziri aeleza sababu
Video: Namna ya kuepukana na msongo wa mawazo, miguu kuvimba, kansa