Jarida la Forbes limemtaja tena Mfanyabiashara Mohammed Dewji katika orodha ya mabilionea wachache Afrika, akishika nafasi ya 16, ingawa utajiri wake umepungua ikilinganishwa na mwaka jana.

Kwa mujibu wa jarida hilo, Mo mwenye umri wa miaka 44 ana ukwasi wa $1.6 Bilioni (sawa na Sh 3.96 trilioni za Kitanzania), huku ikielezwa kuwa ukwasi wake umepungua kwa $300 milioni (Sh692.67 bilioni).  Mwaka jana, Mo alitajwa katika nafasi ya 14.

Mo ameiwakilisha vizuri Tanzania, akiwa ni Mtanzania pekee aliyeingia kwenye orodha hiyo ambayo imeshuhudia nchi nane (8) pekee kati ya nchi 54 za Afrika zilizotoa mabilionea kwenye orodha hiyo. Misri na Afrika Kusini zote zimetoa mabilionea watano kila moja, Nigeria ikifuata kwa kuwa na mabilionea wanne na Morocco wawili. Tanzania, Algeria, Angola na Zimbabwe wao wametoa bilionea mmoja mmoja.

Kilichoendelea kumuweka juu Mo Dewji ni biashara kupitia makampuni yake ya METL ambayo yanafanya kazi katika nchi zaidi ya sita Afrika, kazi kubwa ikiwa kuzalisha bidhaa za unga, vinywaji, mafuta na bidhaa zitokanazo na zao la pamba.

Nafasi ya kwanza imeendelea kushikiliwa na raia wa Nigeria, Aliko Dangote akiwa na ukwasi wa $10.1 Bilioni (sawa na Sh 23.31 trilioni), hadi kufikia Januari 14, 2020, lakini hadi leo anaonekana kupanda hadi $10.2 Bilioni.

Dangote ni Mwenyekiti na mmiliki kwa asilimia 85 wa Makampuni ya Dangote Cement, ambayo yanakadiriwa kuwa huzalisha takribani tani milioni 46 za saruji kwa mwaka. Pia, ana makampuni ya kuzalisha chumvi, sukari na unga wa chakula. Hivi sasa anajenga kiwanda cha Mafuta kinachotajwa kuwa kitakuwa moja kati ya viwanda vikubwa zaidi vya mafuta duniani.

Wanawake wawili pekee ndio waliopata nafasi ya kuingia kwenye orodha hiyo kati ya mabilionea 20. Isabel dos Santos ambaye ni binti mkubwa wa aliyekuwa rais wa Angola, Jose dos Santos, yeye anashika nafasi ya 14 akiwa na utajiri wa $2.2 bilioni. Na mwingine ni raia wa Nigeria, Folorunsho Alakija Kampuni ya mafuta ya Famfa Oil. Yeye anashika nafasi ya 20, akiwa na ukwasi wa $1 bilioni.

Hasara 10 na faida 5 za kuchepuka katika ndoa
Video: Lukuvi ashitukia dili, Utajiriwa wa MO waporomoka kwa dola milioni 300