Mbunge wa Kibamba ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Bara, John Mnyika amewatofautisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Wilbroad Slaa na Katibu Mkuu wa sasa wa chama hicho, Dkt. Vincent Mashinji.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Dar24 ofisini kwake wiki hii, Mnyika amesema kuwa wanasiasa hao ni watu wawili tofauti na waliofanya kazi katika mazingira tofauti na yanayohitaji mbinu tofauti.

“Dkt Slaa ni kwamba alikuwa Mbunge, alikuwa mgombea urais. kwahiyo ana aura ya ubunge na ugombea urais. Upande wa Dkt. Mashinji, sio mbunge, sio mgombea urais lakini ni mtaalam mbobezi na msimamizi wa kiutendaji na makao makuu ya chama,” Myika ameiambia Dar24.

Ameongeza kuwa katika kipindi hiki ambacho mikutano ya hadhara [kwa walioshindwa] imezuiwa na kuna hali tofauti ya kisiasa ukilinganisha na kipindi Dkt. Slaa alipokuwa Katibu Mkuu, mbinu za ziada zinahitajika kufanya siasa kwa vyama vya upinzani ambazo amedai Dkt. Mashinji ni mtu sahihi zaidi kwa wakati huu.

Alisema inahitajika kufanya kazi kimkakati chini kwa chini nchi nzima na kutumia mitandao ya kijamii zaidi pamoja na njia nyingine mbadala.

“Naamini sekretarieti ya sasa hapa tulipo inafanya mapambano katika njia tofauti sana. Tunapofanya mapambano kwa mbinu tofauti, kwa mtu aliyezoea zile mbinu za zamani anaweza kuita ‘tofauti’,” alisema.

Katika hatua nyingine, alikosoa uamuzi wa Dkt. Slaa kukitosa chama hicho wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015 akieleza kuwa alichofanya ni usaliti wa mapambano waliyokuwa wanayaendeleza. Alisema uamuzi huo wa Dkt. Slaa ni moja kati ya vitu ambavyo vilimshangaza zaidi mwaka 2015.
Angalia mahojiano yote hapa:

Marekani yaingilia mgogoro wa kisiasa Ethiopia
Video: Nitashtaki kwa Mungu- Mama 'Sugu', Maaskofu TEC wajilipua