Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amewashukia vikali wanasiasa nane wa Kata ya Kitwai Wilayani Simanjiro wanaorudisha nyuma maendeleo kwa kukataza wanafunzi wasisome kwenye madarasa ya shule ya msingi Kitwai B yaliyojengwa na mdau wa maendeleo hivyo kuyasusia.
 
Ametoa onyo hilo mkoani humo wakati akizindua madarasa matatu mapya ya shule hiyo, ambapo amesema kuwa wanasiasa hao atawachukulia hatua kali wanaoshawishi wananchi kususia maendeleo.
 
Amesema kuwa hatakubali kuona watu wachache wanaopinga maendeleo, hivyo serikali itamuunga mkono mdau huyo wa maendeleo, Sanare Mollel ambaye pia ana mpango wa kumalizia majengo ya Zahanati ya kijiji hicho.
 
“Wanasiasa hao wanampinga mdau huyo kwa sababu ni mfugaji mkubwa ambaye amefuata taratibu na kanuni zote za kuingia ndani ya kijiji hicho lakini hajavunja sheria kwani Mtanzania anaruhusiwa kuishi popote,”amesema Mnyeti.
 
Aidha, amesema kuwa haiwezekani mdau wa maendeleo ajitolee kujenga madarasa matatu kisha baadhi ya wanasiasa wanawaambia wananchi wasisomeshe watoto katika shule hiyo.
 
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo, Nyika Shawishi amesema kuwa wapinzani wake wa kisiasa ndiyo wanaosababisha hali hiyo kwani wanaona maendeleo yakifanyika sifa zitakuwa kwake.
 
Naye ofisa elimu ya msingi wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Silvanus Tairo amesema kuwa shule hiyo imegharimu sh. 47.3 milioni ambapo mdau wa maendeleo alijitolea sh30 milioni na nguvu za wananchi zimegharimu sh.12.3 milioni.

LIVE: Ziara ya Rais Magufuli Mbeya baada ya kuwasili akitokea nchini Malawi
Rais wa Sri Lanka afanya mabadiliko ya vikosi vya usalama