Waziri  wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika, amewataka baadhi ya wakuu wa Wilaya na mikoa nchini kuacha kuwaweka ndani watu kwa saa 48 wakati hakuna sheria inayowapa mamlaka hayo.

Mkuchika amewataka wakuu hao wa Wilaya kuacha kutumia mabavu kwenye utendaji wao wa kazi wa kila siku kwa kuwa wakiendelea na tabia hiyo watakuwa wanahatarisha kazi yake ya uwaziri.

Ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akichangia na kueleza kuwa wakuu wa wilaya na mikoa wanapaswa kutumia busara katika kuwaweka ndani raia, ambapo Waziri Mkuchika amesisitiza Wakuu wa Wilaya wasimponze.

“Msiniponze. Mimi nataka Rais Magufuli asinibadili hapa, mimi nataka Rais Magufuli aseme mzee endelea, tuache masuala ya umwamba, nawaomba huko mliko msiniharibie kazi yangu. Mimi ndiye mwenye cheo cha utawala bora, mimi ndiye Waziri mwenye dhamana ya utawala bora, ukiendesha mambo kinyume cha utawala bora unaniharibia kazi,” amesema Mkuchika.

Aidha, akielezea madaraka ya wakuu wa wilaya kuwaweka ndani watu saa 24, lugha iliyotumika ni kwa usalama wake, maana yake mtu ameua mtu, na jamaa zake wamekasirika wanataka kumpiga yule aliyeua na hapo ndipo dhana ya kumweka huyo mtuhumiwa ndani saa 24 inatumika kwa usalama wake.

Hata hivyo, Januari 29, mwaka huu Rais Magufuli akiwa kwenye hafla ya kuwaapisha majaji, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wapya Ikulu jijini Dar es Salaam, aliwataka wakuu wa wilaya aliowateua kwenda kusimamia sheria, kutoitumia vibaya sheria ya kuwaweka watu rumande.

Madiwani wahoji kuhusu Kondomu, 'Haiwezekani zikosekane'
Mkurugenzi wa Itigi atoa kauli kuhusu tuhuma za mauaji kanisani