Mkoa wa Kagera hatimaye umezindua Soko Kuu la Madini ya TIN Wilayani Kyerwa na mara ya kuzinduliwa rasmi soko hilo biashara ya madini ya TIN imeanza kufanyika mara moja katika soko hilo.
 
Akizindua soko Kuu la Madini ya TIN, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema kuwa nia ya Rais John Magufuli kuagiza masoko ya madini kuanzishwa nchini ni kutaka wananchi wanufaike na rasilimali ya madini katika maeneo yao kwa kuwa na mfumo rasmi wa kukusanya, kuhifadhi na kuuza madini katika masoko maalumu.
 
Amesema kuwa Wizara ya Madini imejidhatiti vyema kudhibiti utoroshaji wa madini nchini na ndiyo maana ilianzisha kanuni za masoko ya madini za mwaka 2019 na kufuta kodi mbili za kero za ongezeko la thamani ya asilimia 18% (VAT 18%) na kodi ya zuio ya asilimia 5% (Withholding Tax 5%) ili kuhakikisha kila mtu katika nafasi yake ananufaika.
 
“Uwepo wa Soko la Madini ya TIN Kyerwa utatatua changamoto za bei ya madini haya hasa kwa wachimbaji wadogo ambapo wafanyabiashara hawataruhusiwa kununua madini ya TIN chini ya bei elekezi ya soko la dunia.
Wachimbaji wadogo sasa ni fursa kwenu kunufaika kama mlivyoona leo madini yanauzwa kutokana na bei ya soko la dunia ya leo.”Amesema Nyongo.
 
Aidha, ametoa muda wa mwezi mmoja kuanzia Mei 8, 2019 kwa wachimbaji wote wa madini wenye leseni za uchimbaji kuhakikisha zinafanya kazi na kama muda huo ukipita bila leseni hizo kuwa hai na kufanya kazi wahusika watanyang’anywa na Serikali itazitoa kwa watu wengine ambao wapo tayari kuzitumia kuchimba madini.
 
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenenrali Marco E. Gaguti katika uzinduzi huo amesema kuwa uzinduzi wa soko la madini ya TIN Kyerwa ambalo tayari limeanza kufanya kazi utaziba uvujifu na utoroshaji wa madini ya TIN kwani hakutakuwa na sababu tena ya kutorosha madini ghafi wakati soko ambalo lina bei ya soko la duni lipo.
 
“Nataka kuona wachimbaji wadogo wa TIN mnatajirika katika mkoa wetu, kwa utafiti wa awali ambao ulifanyika bado kuna vitalu saba vya madini ya TIN hapa Mkoani Kagera ambavyo bado havijawai kuchimbwa na namuomba Waziri hapa mbele yenu mara baada ya utaratibu kukamilika nyinyi wachimbaji wadogo mpewe kipaumbele na tutajirike na madini yetu.”Amesema Gaguti.
 
Nao wachimbaji wadogo wa madini ya TIN Wilayani Kyerwa kupitia umoja wao (KAREMA) wameishukuru Serikali kuanzisha Masoko ya Madini nchini hasa soko la madini ya TIN kwani walikuwa wanashindwa kunufaika na kazi yao na kupunjwa na wafanyabiashara wa madini hayo kutokana na kutokuwa na bei elekezi ya kuuza madini yao pia na soko maalum linalojulikana.

Video: Spika Ndugai aishangaa Serikali, Mvua yaleta maafa
LIVE: Yanayojiri Bungeni Dodoma leo Mei 14, 2019